Wananchi Uingereza waendeleza maandamano ya kuiunga mkono Gaza
Maelfu ya watu nchini Uingereza kwa siku ya 15 mtawalia wamemiminika katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kulaani na kupinga jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza.
Waandamanaji kutoka kaumu, mataifa na dini mbalimbali jana Jumamosi walipiga nara na kutangaza mshikamano na raia wa Palestina katika mitaa ya mji mkuu wa Uingereza London na katika miji mingine yenye watu wengi ya nchi hiyo katika fremu ya kile kiilichopewa jina la "Siku ya Kitaifa ya Uchukuaji hatua kwa ajili ya Palestina".
Waandamanaji walikuwa wamebeba bendera za Palestina huku wakiwa na maberamu na vitambaa vilivyokuwa na maandishi yenye nara na shaari kwa ajili ya kusitishwa ukaliaji mabavu wa Israel na kukomeshwa mfumo wa ubaguzi wa Apartheid wa utawala huo haramu.
Waandamanaji pia wameitaka Uingereza isitishe misaada yake ya silaha kwa utawala wa Kizayuni na imfukuze balozi wa utawala huo huko London. Maandamano ya Uingereza ya kuwaunga mkono raia wa Ukanda wa Gaza yamekuwa harakati ya kisiasa licha ya mashinikizo na vizuizi vya serikali ya nchi hiyo kwa ajili ya kuwanyamazisha waungaji mkono wa Palestina.