Feb 04, 2024 02:37 UTC
  • Mashambulizi makubwa dhidi ya Iraq na Syria; Chokochoko mpya za Marekani eneo la Asia Magharibi

Marekani ambayo kwa miaka kadhaa sasa imevuruga amani ya eneo la Magharibi mwa Asia kutokana na uwepo wake wa kijeshi katika eneo hilo ili kufanikisha malengo yake na ya washirika wake, imekuwa ikiyumbisha usalama wa eneo hilo nyeti na muhimu kwa kufanya mashambulizi na uvamizi wa mara kwa mara.

Katika hatua ya karibuni zaidi, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani CENTCOM kwa kifupi, imetangaza kuwa  vikosi vya jeshi la nchi hiyo vimeshambulia maeneo zaidi ya 85 kwa kutumia ndege za kivita zikiwemo ndege za kivita za kwenda masafa marefu zilizoruka kutoka Marekani. CENTCOM imedai kuwa, katika mashambulizi hayo vikosi vya Marekani vimevishambulia vituo vya uongozaji na udhibiti, vituo vya ujasusi, roketi na makombora na maghaka ya ndege zisizo na rubani (droni) na taasisi za kusambaza silaha kwa makundi ya muqawama huko Iraq na Syria; ambavyo, kwa mujibu wa madai ya kamandi hiyo ya Marekani, vimekuwa vikifanikisha utekelezaji wa mashambulizi dhidi ya vikosi vya nchi hiyo na muungano wa wanajeshi waitifaki wake.  

Hujuma ya anga ya Marekani huko Syria na Iraq 

Ikulu ya Rais wa Marekani (White House) pia imedai kwamba mashambulizi hayo ni jibu kwa mashambulizi ya karibuni dhidi ya kambi yake ya kijeshi. Wanajeshi 3 wa Marekani waliuawa na wengine 34 kujeruhiwa Jumapili iliyopita katika shambulio la droni dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani ya "Mnara wa 22" inayopatikana karibu na mpaka wa Jordan na Syria. Katika taarifa aliyoitoa, Rais Joe Biden ameashiria mashambulizi ya vikosi vya jeshi la nchi huko Iraq na Syria na kudai kuwa maeneo yaliyoshambuliwa yanatumika kuendeshea mashambulizi dhidi ya Marekani. Biden  amesema mashambulizi hayo yataendelea. Hata hivyo Biden amedai kwamba Marekani haitaki vita katika eneo la Mashariki ya Kati au mahali pengine popote duniani!

Wanajeshi vamizi wa Marekani nchini Jordan 

Hii ni pamoja na ukweli kwamba, Marekani imehusika katika vita vingi katika sehemu tofauti duniani baada ya Vita vya Pili vya Dunia, wakati wa Vita Baridi na baada ya kipindi hichoi. Mashambulizi ya Marekani huko ya Afghanistan na Iraq katika muongo wa kwanza wa karne ya 20 na kukaliwa kwa mabavu nchi hizo mbili si tu kwamba kulisababisha mauaji ya maelfu ya watu wa nchi hizo bali pia kuliandaa mazingira ya kushamiri ugaidi katika eneo la Magharibi mwa Asia.  

Katika hatua iliyofuata, Washington ilianza kuchochea vita nchini Syria baada ya machafuko yaliyoanza  mwaka 2011 kwa kuunda muungano wa nchi za Magharibi na Kiarabu. Machafuko yaliyofadhiliwa na Marekani na washirika wake huko Syria yalisababisha mauaji ya watu wengi huko Syria na Iraq na kuwalazimisha  mamilioni ya raia wa nchi mbili hizo kuwa wakimbizi. 

Katika upande mwingine, Marekani katika kipindi cha miaka 70 iliyopita imekuwa na nafasi kubwa katika kuuhami na kuuunga mkono kwa pande zote utawala wa Kizayuni wa Israel unaotekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Palestina; na umedhihirisha waziwazi uungaji wake mkono usio na masharti kwa utawala huo katika vita vya sasa huko Gaza kupitia njia ya kuupatia misaada ya silaha na himaya ya kisiasa na  pia kwa hatua yake ya kuyapiga veto maazimio ya Baraza la Usalama la UN yalilotaka kusimamishwa vita Ukanda wa Gaza.  

Suala  muhimu ni kuwa, mashambulizi ya anga ya Marekani dhidi ya ngome za makundi ya muqawama huko Iraq na Syria yametekelezwa katika hali ambayo kwa upande mmoja eneo la Magharibi mwa Asia limekuwa likishuhudia vita vya Gaza na uungaji mkono wa pande zote wa Washington kwa utawala wa Kizayuni; na kwa upande wa pili eneo hili lilishuhudia majibu ya Mhimili wa Muqawama dhidi ya chokokocho za Marekani ambayo unafanya mashambulizi katika Bahari Nyekundu dhidi ya meli zenye mfungamano au zinazoelekea upande wa utawala wa Kizayuni na pia mashambulizi dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani. Mashambulizi haya yanafanyika ili kuishinikiza Marekani na mwanaharamu wake, Israel, wasimamishe amauaji ya kimbari huko Palestina.

Vita vya Gaza vilivyoanzishwa na utawala haramu wa Israel 

Pamoja na kuwa mwezi wa nne wa vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza unapita sasa, lakini Marekani inaendelea kuunga mkono waziwazi mauaji na uhalifu unaofanywa na Israel. Makundi ya Muqawama ya Kiislamu katika eneo la Magharibi mwa Asia yakiwemo ya huko Iraq na Syria pamoja na vikosi vya wapiganaji wa kujitolea vya wananchi wa Yemen kufuatia mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na uungaji mkono wa pande zote wa Washington kwa utawala huo, viliitahadharisha Marekani kuwa vitashambulia kambi za kijeshi za nchi hiyo katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Makundi ya Muqawama katika eneo hilo ikiwemo huko Iraq, yametangaza mara kwa mara kwamba mashambulizi yao dhidi ya vituo vya Marekani nchini Iraq na Syria ni kwa ajili ya kujibu uungaji mkono mkubwa wa Washington kwa Tel Aviv. Makundi hayo yamekuwa yakisisitiza mara kwa mara kwamba, mashambulizi hayo yataendelea hadi pale Marekani itakapobadili sera zake katika uwanja huo na kuulazimisha utawala wa Kizayuni kusimamisha mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza huko Palestina. 

Wakati huo huo, Washington imekuwa ikijaribu kuihusisha Iran na mashambulizi ya makundi ya Muqawama dhidi ya kambi zake za nchi hiyo na maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Mkabala wake Iran imetangaza mara kadhaa kuwa uungaji mkono wake kwa makundi ya Muqawama huko Palestina na maeneo mengine ni katika fremu ya haki halali ya Muqawama ya kujilinda na kukabiliana na vikosi vamizi na ghasibu. 

Tags