Marekani yafanya kimya kimya mauzo 100 ya silaha kwa Israel
Ripoti mpya imefichua kuwa, Marekani imeidhinisha kimya kimya mauzo 100 ya silaha kwa Israel tangu utawala huo wa Kizayuni uanzishe vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza Oktoba 7, 2023.
Gazeti la Washington Post limeripoti kuwa, maafisa wa Marekani hivi karibuni waliiambia Kongresi ya nchi hiyo katika kikao cha faragha kuwa, mauzo hayo yanajumuisha maelfu ya silaha kama vile mabomu, makombora ya kuelekezwa, maroketi, pamoja na silaha nyingine ndogo ndogo.
Imeelezwa kuwa, ni mauzo mawili tu yaliyodhinishwa na Rais Joe Biden wa Marekani ndiyo yaliyotangazwa na kuwekwa hadharani, huku mauzo zaidi ya 90 yakifanyika kinyemela.
Mauzo hayo yanaendelea kufanyika kinyemela katika hali ambayo, wanaharakati wa haki nchini Marekani wamekuwa wakifanya maandamano ya kuitaka serikali ya nchi hiyo isitishe mauzo ya silaha kwa utawala haramu wa Israel.
Waandamanaji hao wamekuwa wakisisitiza kuwa, upelekaji wowote wa silaha kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ambazo zitatumika katika mashambulizi ya ardhini na angani dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza unakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu, na lazima ukomeshwe.
Kadhalika nchi mbalimbali duniani zimekuwa zikiyataka madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani yaache kutuma silaha na zana za kijeshi kwa utawala unaofanya mauaji ya kimbari wa Israel.
Wapalestina zaidi ya 30,700, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameshauawa shahidi hadi sasa kutokana na vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yaliyoanzishwa na utawala dhalimu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza kufuatia Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekelezwa Oktoba 7,2023 na wanamuqawama wa Palestina