Mar 09, 2024 07:20 UTC
  • Mtaalamu wa UN: Mpango wa Biden wa kujenga bandari Ghaza ni wa 'maonyesho' ya uchaguzi

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa wa Haki amepuuzilia mbali mpango wa Rais wa Marekani wa kuanzisha bandari inayodaiwa kuwa na lengo la kuwezesha kuingizwa misaada katika Ukanda wa Ghaza, ulioteketezwa kwa vita vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vikungwa mkono kwa hali na mali na serikali ya Washington.

Alipohutubia bunge la Marekani siku ya Alkhamisi, Joe Biden alisema ameliamuru jeshi la nchi hiyo kuweka bandari kwenye pwani ya Ghaza katika Bahari ya Mediterania. "Gati ya muda itawezesha kuwepo ongezeko kubwa la misaada ya kibinadamu inayoingia Ghaza," alisema Biden katika hotuba yake hiyo.

Hata hivyo Mtaalamu Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki ya Chakula, Michael Fakhri amesema, hatua hiyo anayokusudia kuchukua rais wa Marekani ni ya jaribio la kuvutia uungaji mkono ndani ya nchi hiyo wakati uchaguzi wa rais ukiwa unakaribia.

Fakhri amebainisha kuwa, hakuna aliyeomba gati ya baharini; si watu wa Palestina, wala si jumuiya inayohusika na misaada ya kibinadamu.

Michael Fakhri

Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa ametamka bayana kuwa, si gati wala si matone ya misaada iliyodondoshwa na Marekani hivi karibuni huko Ghaza, ambayo Wapalestina na waungaji mkono wao wameyadhihaki kuwa ni ya kimaonyesho tu, yatazuia njaa na dhiki ya chakula kwa tafsiri yoyote ile.

Fakhri amekumbusha kuwa, mbinu kama hizo za utoaji misaada (kupitia angani) kwa kawaida hutumika kama suluhisho la mwisho kabisa.

Hayo yanajiri huku zaidi ya Wapalestina 30,800, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wakiwa wameshauawa shahidi hadi sasa katika vita vya kikatili vya mauaji ya kimbari yanayoendelezwa na jeshi la Kizayuni dhidi ya Ghaza.

Tangu vita hivyo vilipoanza tarehe 7 Oktoba, 2023 vimekuwa vikiungwa mkono kikamilifu kisiasa, kijeshi na kijasusi na utawala wa Marekani.

Wakati huo huo, Fakhri ameushutumu utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuendeleza "kampeni ya njaa" huko Ghaza, ambako Umoja wa Mataifa umeonya kuwa, kuzuka kwa baa la njaa ni jambo "lisiloweza kuepukika."

Amefafanua kwa kusema: "nadhani ni sawa kusema sasa kwamba Israel imekuwa ikiwatesa kwa njaa makusudi watu wa Palestina huko Ghaza," na akaongeza kuwa, "sasa hivi kila mtu huko Ghaza anakabiliwa na njaa".../

 

Tags