Mar 20, 2024 11:32 UTC
  • UN: Wahalifu wanachuma dola bilioni 236 kila mwaka kwa biashara ya ngono na utumwa

Utumikishaji binadamu kwenye sekta ya uchumi binafsi ikiwemo biashara ya ngono, viwandani na kwenye mashamba huingiza dola bilioni 236 za faida isiyo halali kila mwaka. Hayo yameelezwa katika ripoti mpya na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi Duniani, ILO.

Ripoti hiyo yenye anuani: Faida na Umasikini: Uchumi wa Utumikishaji, inakadiria kuwa, inakadiria kuwa faida hiyo imeongezeka kwa dola bilioni 64 sawa na asilimia 37 tangu mwaka 2014, na kwamba ongezeko hilo limechochewa na kuongezeka kwa idadi ya watu wanaotumikishwa, na faida kubwa itokanayo na utumikishaji binadamu kwenye sekta mbali mbali. 

Mkuu wa ILO wa Kitengo cha Utafiti na Tathmini Michaelle De Cock amesema, utumikishaji uko kwenye sekta ya umma na ile ya binafsi lakini ile ya umma ni asilimia 27 ilhali sekta binafsi ni asilimia 73.

De Cock amefafanua maana ya faida isiyo halali kuwa ni kiwango cha fedha kinachosalia baada ya kuondoa ujira wa mtumikishwaji kwenye thamani halisi ya kazi aliyoifanya.

Michaelle De Cock

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya ILO, mapato ya mwaka yasiyo halali kutokana na utumikishaji yalikuwa ya juu zaidi Ulaya na Asia ya Kati kwa dola bilioni 84, Asia na Pasifiki zikishika nafasi ya pili kwa dola bilioni 62, Amerika ya tatu dola bilioni 52 huku Afrika ikichukua nafasi ya nne kwa dola bilioni 20 na nchi za Kiarabu dola bilioni 18. 

Imeelezwa kuwa, watumikishaji hujipatia dola 10,000 kwa kila muathiriwa, ikiwa ni ongezeko kutoka dola 8,269 muongo mmoja uliopita.

Utumikishaji kwenye biashara ya ngono ndio unabeba asilimia 73 ya faida yote isiyo halali licha ya waathiriwa kwenye sekta hiyo wakiwa ni asilimia 27 tu ya watumikishwaji wote. 

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa ILO Gilbert F. Houngbo amesema, utumikishwaji kwenye ajira unaendeleza mzunguko wa umaskini na unyonyaji na unatokomeza na kurarua utu wa kibinadamu.

Ameongezea kwa kusema: "tunafahamu kwamba hali imezidi kuwa mbaya. Jamii ya Kimataifa lazima iungane na kuchukua hatua kumaliza ukosefu huu wa haki”.../ 

 

Tags