Msomi Myahudi akosoa vikali UN kushindwa kuchukua hatua juu ya Ghaza kutokana na kura za veto
Mtengenezaji filamu mashuhuri wa Kiyahudi Haim Bresheeth, ambaye pia ni mpiga picha na msomi mtajika amekosoa vikali Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kushindwa kuchukua hatua katika mzozo wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Palestina kutokana na kura ya turufu inayoshikiliwa na wanachama wake watano wa kudumu.
Ameeleza pia kwamba amekamilisha filamu aliyotengeneza kuhusu hali ya Ghaza, hata hivyo amesema ana shaka kama itaweza kuonyeshwa nchini Uingereza kutokana na muelekeo wake wa kupinga Uzayuni.
Profesa Bresheeth amevikosoa pia vyombo vya habari vya Magharibi kwa kupuuza mateso ya Wapalestina na kuakisi zaidi uungaji mkono wa Magharibi kwa Israel licha ya kushutumiwa kwa mauaji ya kimbari.
Halikadhalika, msomi huyo amezungumzia kutimuliwa wasomi na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuzungumza dhidi ya mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo huko Ghaza na akasema, muelekeo sawa na huo unafuatwa nchini Uingereza, ambako vyuo vikuu vimewafukuza maprofesa kadhaa na kuchukua hatua dhidi ya wanafunzi pia.
“Nina maprofesa kadhaa ninaowajua waliofukuzwa kazi Israel kwa sababu wamesema kinachoendelea Ghaza si ubinadamu na hakipasi kuungwa mkono kwa vyovyote vile. Nchini Uingereza, vyuo vikuu vimewafukuza kazi maprofesa kadhaa na kuchukua hatua dhidi ya wanafunzi, wengi wao wakiwa ni Wapalestina na Wayahudi, ambao wameandamana kupinga vita, wakitaka kusitishwa mapigano".../