Mar 29, 2024 07:41 UTC
  • ICJ: Israel lazima ihakikishe msaada wa dharura, chakula vinaingizwa Ghaza bila kuchelewa

Mahakama ya Juu zaidi duniani ya Haki ICJ imeuamuru utawala wa Kizayuni wa Israel "kuhakikisha msaada wa haraka wa kibinadamu" unaingizwa huko Ghaza bila kuchelewa, ikisisitiza kuwa "njaa imeshaingia" katika eneo hilo.

Katika agizo ililotoa hapo jana Alkhamisi ICJ imesema: "Israel ichukue hatua zote muhimu na madhubuti ili kuhakikisha, bila kuchelewa, utoaji usiozuiliwa wa huduma za kimsingi zinazohitajika haraka na usaidizi wa kibinadamu unafikishwa huko Ghaza".
 
Uamuzi wa mahakama hiyo yenye makao yake The Hague, Uholanzi umesisitiza kuwa: "Wapalestina huko Ghaza hawakabiliwi tena na hatari ya njaa tu, lakini njaa ipo sasa na inazidi".
 
Vita vya kikatili na mauaji ya kinyama ya kimbari yanayoendelea kufanywa mtawalia kwa mwezi wa sita sasa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel, hadi sasa vimeshateketeza roho za watu wasiopungua 32,552 katika Ukanda wa Ghaza wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Hali ya Ghaza

Mahakama ya ICJ imetoa agizo hilo kwa utawala wa Kizayuni huku waziri mkuu wa utawala huo Benjamin Netanyahu akitangaza kuwa jeshi linajiandaa kwa operesheni ya kuuvamia mji wa Rafah ulioko kusini mwa Ghaza, ambao umehifadhi Wapalestina zaidi ya milioni moja na laki tatu ambao walitakiwa na jeshi la Kizayuni waelekee huko kwa ajili ya kupata hifadhi.

 
Netanyahu ameeleza katika taarifa kwamba, baada ya kuyavamia na kuyakalia maeneo ya kaskazini ya Ukanda wa Ghaza na Khan Yunis, uvamizi wa kijeshi katika mji wa Rafah unafuatia.../

Tags