Apr 19, 2024 07:29 UTC
  • Marekani yalipigia kura ya veto azimio la kuipatia Palestina uanachama kamili wa Umoja wa Mataifa

Marekani, ambayo ni muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, imeendeleza sera yake ya kudhoofisha kupatikana haki za Wapalestina kwa kutumia vibaya haki yake ya kura ya turufu na kukwamisha azimio la kuipatia Palestina uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa IRNA, Algeria iliwasilisha kwa Baraza la Usalama, rasimu ya azimio la uwanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, na kikao cha baraza hilo cha kupigia kura azimio hilo kilifanyika Alhamisi jioni kwa saa za New York.

Katika upigaji kura huo, nchi 12 wanachama wa Baraza la Usalama la UN zilipiga kura za kuunga mkono, Uswisi na Uingereza zilipiga kura ya kutopinga au kuunga mkono upande wowote; na Marekani ikazuia kupitishwa azimio hilo kwa kulipigia kura ya turufu.

Kwa hatua yake ya sasa ya kulipigia kura ya turufu azimio la kuipatia Palestina uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa, kwa mara nyingine tena Marekani imeonyesha kwamba madai yake kuwa inaiunga mkono Palestina na watu wake wanaodhulumiwa si chochote zaidi ya maneno matupu na haiko tayari hata kupiga kura kuunga mkono uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa.

Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia ametoa mjibizo kwa hatua ya Marekani ya kutumia kura yake ya turufu kupinga uwanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa na kusema kuwa, lengo la Marekani ni kuvunja irada ya Wapalestina na kuwafukuza katika ardhi yao.

Kwa sasa, Palestina mtazamaji wa kudumu katika Umoja wa Mataifa. Mnamo mwaka 2011, taifa hilo madhulumu liliomba uanachama wa kudumu katika umoja huo.

Mwezi Aprili, Palestina ilituma barua kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiomba lifikirie upya ombi lake la kujiunga na Umoja wa Mataifa kwa sura ya mwanachama wa kudumu.../

Tags