Nchi za Amerika ya Kusini zaunga mkono Palestina
Wanachama wa Muungano wa ALBA huko Amerika ya Kusini wameunga mkono muqawama wa Palestina dhidi ya mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni.
Wanachama wa Muungano wa Eneo la ALBA unaojumuisha nchi kumi za Amerika ya Kusini (Amerika ya Latini) sanjari na kulaani mauaji na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita wamesema kimya na ushirikiano wa nchi za Magharibi na utawala katili wa Israel ndio sababu ya kuendelea na kuongezeka jinai hizo.
Nchi wanachama wa "Muungano wa Bolivari kwa ajili ya Watu wa Amerika, Mkataba wa Biashara wa Watu Wetu" unaojulikana kwa ufupi kama ALBA, pia wametangaza rasmi mshikamano wao wa dhati na taifa la Palestina.
Wanachama wa Muungano wa ALBA wamesema mauaji ya kiholela ya makumi ya maelfu ya raia hususan watoto na wanawake wasio na hatia ni jinai isiyoweza kuhalalishwa na kwamba mauaji ya kimbari ya mwaka mmoja uliopita ya utawala wa Kizayuni ni jinai na kitendo cha kinyama ambacho kinatishia usalama wa nchi zote za Asia Magharibi.
Nchi wanachama wa ALBA pia zimesifu, kutambua na kuunga mkono nguvu za watu wa Palestina na azma yao ya kupinga na kusimama imara mbele ya mauaji ya kimbari ya Israel yanayotekelezwa kwa uungaji mkono wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya.
Wanachama wa Umoja wa ALBA wametangaza kuwa, muqawama wa Palestina uko hai zaidi kuliko wakati mwingine wowote licha ya miaka 76 ya ukaliaji mabavu unaokiuka sheria, machungu, mauaji na uharibifu wa Wazayuni. Venezuela, Cuba, Bolivia na Nicaragua ni miongoni mwa wanachama kumi wa Muungano wa Kikanda wa ALBA katika Amerika ya Kusini.