Sheria za kupambana na ugaidi Uingereza zatumiwa kunyamazisha wanaopinga Israel
(last modified 2024-10-19T11:25:52+00:00 )
Oct 19, 2024 11:25 UTC
  • Sheria za kupambana na ugaidi Uingereza zatumiwa kunyamazisha wanaopinga Israel

Polisi wa Uingereza wanaopambana na ugaidi wamevamia nyumba ya mwandishi wa habari za uchunguzi na mtafiti, Asa Winstanley, Kaskazini mwa London.

Takriban maafisa kumi walifika nyumbani kwa Winstanley kabla ya saa kumi na mbili asubuhi ya Ijumaa na kumuonyesha vibali vilivyowaidhinisha kupekua nyumba na gari lake ili kutafuta vifaa na hati.

Maafisa walimfahamisha mhariri huyo wa tovuti ya habari ya Electronic Intifada kwamba uvamizi huo unahusishwa na machapisho ya mtandaoni ambayo alikuwa ameyachapisha, na kwamba anachunguzwa kwa uwezekano kuwa eti amehimiza ugaidi. Winstanley, hata hivyo, hakukamatwa na bado hajafunguliwa mashtaka yoyote.

Wateetezi wa haki za binadamu wanasema uvamizi huo ni mfano mwingine wa serikali ya Uingereza kujaribu kuwakakndamiza na kuwabana wale wote wanaopinga utawala katili wa Israel na kuwatia hofu watu wengine wasizungumze kuhusu ukatili usio na mwisho wa utawala huo ghasibu.

Massoud Shadjareh wa Kamisheni ya Haki za Kibinadamu ya Kiislamu yenye makao yake mjini London, amesema sheria ya ugaidi imekuwa ikitumiwa vibaya kila wakati, na kwa bahati mbaya, sasa tunaiona ikitumiwa vibaya dhidi ya mwandishi wa habari. Amesema watetezi wa haki za binadamu wasiruhusu jambo hilo lifanyike tena.

Uvamizi kwenye nyumba ya Asa Winstanley ni mfano wa hivi karibuni tu wa sheria ya kukabiliana na ugaidi inayotumiwa vibaya dhidi ya waandishi wa habari huru katika nchi ambayo inadai kuwa kimbilio salama kwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa wanahabari.

Hata hivyo katika miezi ya hivi karibuni, Uingereza imetumia mamlaka makubwa dhidi ya waandishi wa habari mashuhuri kama vile Kit Klarenberg na Richard Medhurst pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu kama vile Sarah Wilkinson.

Wanaharakati wanahofia kwamba aina hii ya uvamizi inalenga kunyamazisha upinzani wote dhidi ya uhalifu unaofanywa na Israel na kuufanya kuwa wa kawaida machoni pa ulimwengu.