Rais wa China ayataka majeshi yajizatiti zaidi katika kujiweka tayari kwa vita
Rais Xi Jinping wa China ametoa wito kwa majeshi ya nchi hiyo kujizatiti zaidi katika kujiweka tayari kwa vita, siku chache baada ya Beijing kufanya mazoezi makubwa ya kijeshi kuzunguka kisiwa chaTaiwan.

Katika miaka ya karibuni, China, ambayo inasisitiza kuwa Taiwan ni sehemu ya ardhi yake, imezidi kutunisha misuli ya nguvu zake za kijeshi kuzunguka kisiwa hicho kinachojitawala.
Siku ya Jumatatu, Beijing ilituma ndege za kivita, ndege zisizo na rubani, manowari na meli za gadi ya pwani kuizunguka Taiwan, ikiwa ni duru yake ya nne ya mazoezi makubwa ya kivita kuzunguka kisiwa hicho ndani ya kipindi cha miaka miwili tu.
Viongozi wa China wameshasisitiza kuwa hawaondoi uwezekano wa kutumia nguvu ili kuirejesha Taiwan chini ya udhibiti wa nchi hiyo.
Mzozo kati ya China na Taiwan ulianza katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ambapo vikosi vya kitaifa vya Chiang Kai-shek vilishindwa na wapiganaji wa kikomunisti wa Mao Zedong na kukimbilia kwenye kisiwa hicho mnamo mwaka1949.
Tangu wakati huo, China na Taiwan zimekuwa zikitawaliwa na uongozi tofauti.../