Mapambano dhidi ya ugaidi, ni wasiwasi mkuu wa wananchi wa Ufaransa
Taasisi moja inayojihusisha na uchunguzi wa maoni ya ufaransa imeeleza kuwa suala la kuendesha mapambano dhidi ya ugaidi ni jambo linalowatia wasiwasi sana wananchi wa Ufaransa.
Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Taasisi ya Kifaransa ya Ifop ambao umechapishwa Jumatano wiki hii umeonyesha kuwa asilimia 67 ya watu walioshiriki kwenye uchunguzi huo wa maoni wanaamini kuwa, vita dhidi ya ugaidi ni kadhia inayowatia wasiwasi mkubwa raia wa Ufaransa hadi kufanyika uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo mwaka 2017.
Kwa mujibu wa matokeo ya taasisi hiyo ya utafiti wa maoni, suala la ukosefu wa ajira na uboreshaji wa hali ya uchumi huko Ufaransa, ni miongoni mwa kadhia nyingine zinazowatia wasiwasi wananchi. Ripoti ya taasisi hiyo ya uchunguzi wa maoni ya Ifop imeonyesha pia kuwa suala la kupambana na ugaidi ni moja ya mambo muhimu yanahusu uchaguzi mkuu ujao nchini Ufaransa.
Tafiti hizo zilifanyika kati ya tarehe 21 hadi 25 mwezi huu, baada ya shambulio la Julai 14 katika mji wa Nice kusini mashariki mwa Ufaransa.