Russia kushirikiana na US kwenye faili la nyuklia la Iran
Russia imeeleza nia ya kushirikiana na Marekani katika kushughulikia masuala ya Asia Magharibi, ikiwa ni pamoja na mradi wa nyuklia wa Iran, ikizingatiwa kuwa uhusiano wa Moscow na Washington unazidi kuimarika.
Gazeti la Haaretz siku ya Jumapili lilimnukuu Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova, akisema kuwa mtazamo wa pamoja kwa makubaliano ya nyuklia ya Iran ya mwaka 2015, unaoitwa rasmi Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA), unaweza kuwa na manufaa kwa ajili ya kuleta utulivu kuhusiana na Iran.
Pia amesema kuwa Russia "haifuti uwezekano" kwamba Iran itakubali kwa mara nyingine kupunguza shughuli zake za nyuklia mkabala wa kuondolewa vikwazo vinavyoongozwa na Marekani.
Alipoulizwa iwapo Russia itatumia ushawishi wake kupunguza au kusimamisha mpango wa nyuklia wa Iran, Zakharova alilikumbusha gazeti hilo la Israel kwamba, Iran haina nia ya kutengeneza silaha za nyuklia na kwamba mradi wake huo ni wa nishati ya nyuklia kwa madhumuni ya kiraia tu.
"Tumejitayarisha kwa ushirikiano wa karibu zaidi na Tehran na pande zingine zinazohusika kwa ajili ya kupunguza mvutano na kutafuta masuluhisho endelevu yatakayowezesha makubaliano yenye ufanisi na ya muda mrefu," ameongeza Zakharova.
Huko nyuma mwaka 2018, wakati huo Donald Trump akihudumu muhula wa kwanza wa urais, kwa upande mmoja aliiondoa Washington katika mapatano ya JCPOA na kuanzisha sera ya "mashinikizo ya juu zaidi" dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.