Kukiri jamii ya ujasusi ya Marekani kwamba Hamas haijashindwa huko Gaza
Ripoti kuhusu vitisho ambayo hutolewa kila mwaka na jamii ya masuala ya ujasusi ya Marekani imekiri kwamba kundi la muqawama wa Palestina la Hamas huko Gaza halijashindwa bado na kwamba linaendelea kudumisha nguvu, wapiganaji na miundombinu yake.
Ripoti ya jamii ya ujasusi ya Marekani, imeeleza kuwa: "Kundi hilo lina maelfu ya wanajeshi na kwamba miundombinu yake mingi ya chini ya ardhi ingali ipo imara, na kuna uwezekano limetumia kipindi cha usitishaji vita kuimarisha na kukarabati silaha zake ili liweze kupigana tena." Tathmini hiyo inaongeza kuwa Hamas inaweza kuanzisha tena mapambano ya chini kwa chini na kubakia kuwa kigezo kikuu cha kisiasa huko Gaza katika siku zijazo. Ripoti hiyo inadai kuwa umaarufu wa Hamas umepungua katika ukanda huo, lakini umaarufu wake katika Ukingo wa Magharibi, "hasa ndani ya Mamlaka ya Utawala wa Ndani ya Palestina" bado uko juu.
Ripoti ya jamii ya kijasusi ya Marekani kuhusu hali ya Hamas kwa mara nyingine inaonesha kuwa licha ya madai ya utawala wa Kizayuni kuhusu kuharibu sehemu kubwa ya vikosi, zana na hata mahandaki ya Hamas katika Ukanda wa Gaza, lakini kundi hili la muqawama wa Palestina bado lina uwezo mkubwa wa kijeshi na limeweza kulinda nguvu, wapiganaji na miundombinu yake licha ya mashambulizi ya mfululizo ya Israel katika ukanda huo.
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni alianzisha vita huko Gaza akiwa na malengo manne makuu na maalum. Aliahidi kwamba angesimamisha tu vita hivyo baada ya kutimiza malengo hayo, lakini mkondo wa vita, ulichukua muelekeo tofauti kabisa, kwa uchache kabla ya kuvunjika usitishaji vita wa hivi karibuni. Lengo kuu la Netanyahu lilikuwa ni kufuta kabisa harakati ya Hamas, ikiwa ni pamoja na kuharibu miundombinu yake mikuu na mtandao mpana wa njia za chini ya ardhi. Hata hivyo, Hamas imeweza kuimarisha majeshi yake katika muda mfupi sana katika maeneo ambayo jeshi la Kizayuni lilijiondoa. Ripoti kutoka vyanzo vya Wazayuni na Magharibi zinaonyesha ukweli kwamba jeshi la utawala wa Kizayuni limeshindwa kuvunja nguzo kuu za nguvu ya Hamas.

Lengo la pili la Netanyahu lilikuwa ni kuwakomboa mateka wa Kizayuni kupitia chaguo la kijeshi. Katika uwanja huo, lengo la Wazayuni lilikuwa ni kukomboa makumi ya mateka wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza waliokuwa mikononi mwa vikosi vya Hamas na makundi mengine ya muqawama baada ya siku 471 za vita. Lakini kivitendo jeshi la Kizayuni liliweza kuwakomboa mateka wachache tu wa Kizayuni huko Gaza kupitia operesheni za kijeshi licha ya mashambulizi makali katika ukanda huo, na hivyo kushindwa vibaya katika kutimiza ahadi hii. Hatimaye utawala wa Kizayuni ulilazimika kuwaachilia huru wafungwa 1,737 wa Kipalestina, ambao idadi kubwa kati yao walihukumiwa vifungo vya maisha jela, katika kubadilishana na mateka wake kutoka Gaza, na pia ukalazimika kuwaachilia huru wafungwa wote wanawake na watoto.
Lengo la tatu la Netanyahu lilikuwa ni kupata udhibiti wa kudumu katika ukanda wa Philadelphia na Netsarim. Kwa kuendelea kukaliwa kwa mabavu mhimili wa Philadelphia kwenye mpaka kati ya Gaza na Misri, jeshi la utawala wa Kizayuni lilitumai kukata misaada ya silaha kwa muqawama wa Palestina, na hatimaye utawala huo ukalazimika kukubali kuondoka taratibu katika eneo hilo na vilevile ukanda wa Netsarim.
Lengo la nne la Netanyahu lilikuwa ni kuchukua udhibiti wa Ukanda wa Gaza kwa kuanzisha upya ujenzi wa vitongoji kaskazini mwa Gaza kwa kuzingatia mpango uliowasilishwa na majenerali wa zamani wa jeshi la utawala wa Kizayuni. Kwa kuanzishwa usitishaji vita na kuondolewa jeshi la utawala wa Kizayuni katika maeneo ya makazi ya watu, hamu ya kutaka kujenga vitongoji vya walowezi huko Gaza kwa ajili ya wafuasi wa mrengo wa kulia wa Israel ilitoweka taratibu. Hatimaye wananchi wa Palestina walirejea makwao kaskazini mwa Ukanda wa Gaza. Kwa hiyo, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni ameshindwa kutimiza malengo yake yote aliyoyatangaza rasmi katika kuanzisha vita vya Gaza.
Wakuu wa Hamas pia wamesisitiza suala hili mara nyingi kwamba pamoja na hatua za kiuadui za utawala wa Kizayuni, lakini kundi hili la muqawama bado lina uwezo mkubwa wa kiutendaji na wa kukarabati vikosi na silaha zake. Katika muktadha huu, Sami Abu Zuhri, mmoja wa viongozi wakuu wa Hamas, amesema: Utawala wa Kizayuni unadanganyika kuhusu uwezekano wa kuiangamiza Hamas kwa kuwaua shahidi makamanda wake. Hamas ni vuguvugu ambalo limekita mizizi Palestina na lina makamanda wengi na wala haliwezi kusambaratishwa kupitia vitendo vya ugaidi na jinai za kivita.