Indhari ya WHO kuhusu kushtadi migogoro ya kibinadamu kufuatia kusimamishwa misaada ya Marekani
Afisa mmoja wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Jumapili Aprili 20 alitahadharisha kuwa kupungua misaada ya nje ya Marekani kunaweza kuzidisha ugumu na kutatiza pakubwa migogoro ya kibinadamu kote ulimwenguni.
Hanan Balkhy, Mkurugenzi wa Kanda ya Mediterania ya Mashariki katika Shirika la Afya Duniani amesema: Misaada iliyokuwa ikitolewa kwa timu za matibabu ya dharura, utoaji wa dawa na ukarabati wa vituo vya afya yote imeathiriwa moja kwa moja kufuatia kusitishwa misaada ya kifedha ya Marekani kwa nchi mbalimbali duniani.

Shirika la Afya Duniani ni miongoni mwa taasisi za Umoja wa Mataifa lenye jukumu la kulinda afya ya mwili na akili ya watu duniani na kupambana na magonjwa mbalimbali. Shirika hilo la kimataifa liliundwa mwaka 1948 na ofisi yake kuu ipo nchini Uswisi. Shirika la Afya Duniani lenye nchi wanachama 194 ikiwemo (Marekani) linajihusisha na miradi mbalimbali kama utoaji chanjo, kusaidia watu kupambana na dharura za kiafya na kuzisaidia nchi kutoa huduma za afya kwa wananchi. Shirika hilo pia hushiriki katika kuratibu kanuni za kimataifa kuhusu usalama wa chakula, njia za upimaji dawa na viwango vya matibabu. WHO hupata fedha za kujiendesha kutoka nchi wanachama na misaada ya watu mbalimbali. Bajeti ya shirika hilo kwa mwaka huu wa 2025 Miladia ni dola bilioni 6.83. Marekani ambayo kwa muda sasa imekuwa ikilidhamini pakubwa kifedha Shirika la Afya Duniani haijalipa shirika hilo mchango wake wa fedha wa mwaka uliopita na haijulikani hadi sasa iwapo nchi hiyo itatekeleza jukumu lake la nchi mwanachama kwa ajili ya mwaka huu au la. Hii ni kwa sababu Rais wa Marekani Donald Trump ameamuru kusimamishwa misaada ya nchi hiyo kwa taasisi hiyo ya kimataifa.
Kukataa Marekani kutoa misaada ya fedha kumetatiza shughuli za WHO. Rais Donald Trump wa Marekani amesimamisha misaada ya fedha ya nje ya nchi hiyo tangu aanze muhula wake wa urais Januari mwaka huu; na kuvunja Shirika la Marekani la Misaada ya Kimataifa (USAID) na shughuli nyingine na kusababisha kujiondoa katika WHO.
Donald Trump alianza mchakato wa kuiondoa Marekani katika Shirika la Afya Duniani kwa kutia saini agizo kuu mnamo Januari 21 mwaka huu. Hii ni mara ya pili ambapo Trump anaamuru kuiondoa Marekani katika shirika hilo la kimataifa. Mwishoni mwa muhula wake wa kwanza wa urais mwaka 2020 pia Trump aliituhumu WHO kuwa ilisimamia vibaya janga la mripuko wa Uviko-19 na kuamrisha kujitoa Marekani ndani ya shirika hilo. Trump alikatia WHO misaada ya kifedha akilituhumu kuwa lilipuuza nafasi ya China katika kueneza Corona na kushindwa kukabiliana na janga hilo; na hatimaye tangazo la kujiondoa Marekani katika taasisi hii ya kimataifa lilifutwa wakati wa utawala wa Joe Biden. Trump mara hii pia anadai kuwa kushindwa WHO kutekeleza marekebisho ya dharura na kukosekana uhuru mkabala wa ushawishi wa kisiasa usiofaa wa baadhi ya nchi wanachama ni miongoni mwa sababu za kutolewa agizo hilo la kujitoa ndani ya WHO. Wakati huo huo, Trump amedai kuwa Shirika la Afya Duniani linataka Marekani iipatie fedha nyingi na zisizo za kiadilifu ikilinganishwa na mgawo wa nchi nyingine. Rais wa Marekani ameituhumu waziwazi China kuwa inaingilia kati na kuwa na ushawishi katika shirika hilo.

Kimsingi moja ya viashiria muhimu vya utawala wa Trump ni hatua za upande mmoja na maamuzi yake hasi kuhusu taasisi, makubaliano na mikataba ya kikanda na kimataifa. Donald Trump aliiondoa Marekani katika aghlabu ya taasisi na makubaliano ya kimataifa kama Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Paris, Makubaliano ya Nyuklia ya JCPOA, Mkataba wa Biashara Huru wa Pande Mbili za Pasifiki (TPP) na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa katika muhula wa kwanza wa Urais wake ulioanzia mwezi Januari 2017 hadi Januari 2021.
Kuingia tena madarakani Donald Trump kumehuisha sera ya maamuzi ya upande mmoja na kuzidisha hitilafu kati ya Washington na madola yenye nguvu duniani, na wakati huo huo kuzidisha mashinikizo kwa Umoja wa Mataifa na taasisi zake tanzu, likiwemo Shirika la Afya Duniani. Trump anatumia kaulimbiu ya "Marekani Kwanza" akitoa kipaumbele kwa maslahi na malengo ya Marekani na kuzikosoa nchi nyingine na taasisi za kimataifa. Bila ya shaka, ili kufikia lengo lake hilo yaani Trump amejikita katika kuzitumia taasisi za kimataifa kama wenzo kinyume na maadili mema na ubinadamu yaani kupunguza kwa kasi misaada ya kifedha na pia kutishia kujitoa au kujiondoa kabisa katika taasisi hizo suala mbalo limezidisha kutoaminika nafasi ya Marekani duniani.