Chuo Kikuu cha Harvard chafungua mashtaka dhidi ya utawala wa Trump
(last modified Tue, 22 Apr 2025 07:09:46 GMT )
Apr 22, 2025 07:09 UTC
  • Chuo Kikuu cha Harvard chafungua mashtaka dhidi ya utawala wa Trump

Chuo Kikuu cha Harvard kimefungua mashtaka dhidi ya serikali ya Marekani kikitaka kumzuia Rais Donald Trump asisimamishe mabilioni ya dola ya bajeti ya Serikali ya Federali kwa chuo hicho na kulinda uhuru wake.

Rais wa Marekani Donald Trump alikata bajeti ya serikali kwa vyuo vikuu kama Harvard, Columbia na kadhalika ambavyo anadai vimeshindwa kudhibiti suala la chuki dhidi ya Wayahudi kwenye vyuo hivyo. Wanafunzi na walimu wa vyuo hivyo wamekuwa wakifanya maandamano na migomo wakipinga mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza, Palestina.

Kesi ya Chuo Kikuu cha Harvard dhidi ya Rais wa Marekani, iliyowasilishwa katika mahakama ya shirikisho huko Boston, inasema Trump ameanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya ufadhili wa utafiti wa hali ya juu katika vyuo vikuu vya Marekani kwa madai ya kutokomeza chuki dhidi ya Wayahudi na itikadi kali.

Alan Garber, Rais wa Chuo Kikuu cha Harvard amesema kuongezeka mivutano ya serikali ya Marekani dhidi ya taasisi hiyo ya kifahari kuna madhara makubwa kwa wagonjwa, wanafunzi, wahadhiri, wafanyakazi, watafiti na nafasi ya elimu ya juu ya Marekani duniani.

Tangu aliposhika madaraka mapema mwaka huu, Donald Trump alianzisha kampeni kubwa ya kunyamazisha sauti zote zinazopinga sera za utawala katili wa Israel na maandamano yanayofanywa na wanafunzi wa vyuo vikuu kupinga mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israe huko Palestina hususan katika Ukanda wa gaza.