Sep 22, 2016 04:25 UTC
  • UN yataka msaada wa Iran kuhusu migogoro ya Syria, Yemen

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametaka msaada wa Iran katika kutafutia suluhisho la kudumu migogoro inayotokota Syria na Yemen.

Ban amewasilisha ombi hilo wakati alipokutana na Rais Hassan Rouhani wa Iran Jumatano pembizoni mwa Mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.

Katika kikao hicho kifupi, Ban alimuomba Rais Rouhani atumie ushawishi wake  kuhuisha mchakato wa amani katika nchi hizo mbili.

Ban pia alisisitiza umuhimu wa pande zote kutekeleza kikamilifu mapatano ya nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa duniani ambayo ni maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA)

Rais Rouhani (kushoto) na Ban Ki-moon

Ikumbukwe kuwa Julai 2015, Iran na nchi za 5+1 ambazo ni Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Russia na Marekani zilitiliana saini mapatano ya nyuklia ambapo Tehran ilitakiwa ipunguze baadhi ya shughuli zake za nyuklia mkabala wa kuondolewa vikwazo ilivyowekewa kutokana na shughuli hizo za nyuklia.

Kwa upande wake, Rais Rouhani amebainisha wasiwasi wake kuhusu hujuma za kijeshi  zisizo na kikomo za Saudi Arabia pamoja na jinai za utawala huo wa Riyadh dhidi ya raia. Amesema, pamoja na kuwepo mashinikzo, Umoja wa Mataifa haupaswi kuacha majukumu yake ya kutetea haki za binadamu Yemen. Aidha Rouhani amesema mgogoro wa miaka mitano Syria hauna suluhisho la kijeshi bali kunahitajika mazungumzo ya kisasa.

 

Tags