Dec 20, 2016 08:03 UTC
  • Kadhaa wajeruhiwa baada ya msikiti kuhujumiwa Zurich, Uswisi

Watu watatu wamejeruhiwa baada ya mtu aliyekuwa na bunduki kushambulia msikiti na kufyatua risasi ovyo akiwalenga waumini waliokuwa wakitekeleza ibada zao katika mji wa Zurich nchini Uswisi usiku wa kuamkia leo.

Marco Bisa, msemaji wa polisi mjini Zurich amethibitisha kutokea hujuma hiyo na kubainisha kuwa, wawili kati ya waliofyatuliwa risasi katika hujuma hiyo wako katika hali mbaya na kwamba wameanza kusaka mhusika wa jinai hiyo. Inaarifiwa kuwa, aliyetekeleza jinai hiyo ni kijana wa miaka 30 hivi, ambaye alifanikiwa kutoroka baada ya kufanya hujuma hiyo. 

Abukar Abshirow, mmoja wa mashuhuda wa shambulizi hilo amesema msikiti huo ambao umepakana na Kituo cha Kiislamu katika barabara ya Eisgasse mjini Zurich, umekuwepo katika eneo hilo tangu mwaka 2012 na kwamba hawajawahi kushuhudia kitendo cha aina hii cha chuki dhidi ya Uislamu.

Mkutano wa kujadili chuki dhidi ya Uislamu ulifanyika hivi karibuni London

Licha ya kuwa kuna Waislamu zaidi ya laki nne nchini Uswisi, lakini katiba ya nchi hiyo mwaka 2009 ilipiga marufuku kujengwa minara zaidi ya minne iliyopo, katika misikiti zaidi ya 150 nchini humo.

Vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu vimeongezeka kwa kiasi kikubwa katika nchi nyingi za Ulaya na Marekani. Hivi karibuni kuta za msikiti mmoja wa eneo la Bron katika mji wa Lyon, nchini Ufaransa ziliandikwa maneno ya kibaguzi na vitisho dhidi ya Waislamu.

Aidha Septemba mwaka huu, Kituo cha Kiislamu katika eneo la Fort Pierce jimbo la Florida nchini Marekani kiliteketezwa moto na watu wenye chuki dhidi ya Uislamu, wakati Waislamu walikuwa wanajitayarisha kusherehekea Siku Kuu ya Idul Adh'ha.

Tags