Vikosi vya jeshi la Marekani vyakiri kuua raia 33 wa Afghanistan
Vikosi vya jeshi la Marekani vilivyoko chini ya mwavuli wa shirika la kijeshi la NATO vimekiri kuwa viliua raia 33 wa Afghanistan wakiwemo watoto wadogo katika shambulio la mwezi Novemba jana lililofanywa kwa kisingizio cha kupambana na wanamgambo wa kundi la Taliban.
Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo leo imekiri pia kuwa raia wengine 27 walijeruhiwa katika shambulio hilo la anga dhidi ya kijiji cha Boz kilichoko kwenye mji wa Kunduz kaskazini mwa Afghanistan.
Kamanda wa jeshi la Marekani katika shirika la NATO Jenerali John Nicholson amedai kupitia taarifa hiyo kuwa operesheni ya shambulio hilo la Novemba 3 ililenga kuwakamata makamanda wa Taliban ambao kwa mujibu wa Washington walihusika katika shambulio lililofanywa na kundi hilo mwezi Oktoba mwaka 2015 la kuyateka baadhi ya maeneo ya mji wa Kunduz.
Mauaji hayo ya raia yalilaaniwa na Umoja wa Mataifa na jumuiya za misaada ya kibinadamu.
Baada ya mauaji hayo ya kinyama, wakaazi wa kijiji cha Boz walibeba makumi ya maiti zikiwemo za watoto hadi ofisi ya Gavana wa eneo hilo kuonyesha hasira na uchungu waliokuwa nao.
Mkaazi mmoja wa kijiji cha Boz aliyepoteza jamaa kadhaa wa familia yake katika shambulio dhidi ya kijiji hicho amesema shambulio hilo liliua raia tu wasio na hatia; na nyumba za raia hao zililengwa moja kwa moja kwa kutegemea taarifa za dhana tu.
Marekani iliivamia na kuishambulia kijeshi Afghanistan mwaka 2001 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Japokuwa uvamizi huo uliwezesha kuliondoa madarakani kundi la Taliban lakini Amani haijarudi tena katika nchi hiyo huku machafuko na umwagaji damu yakiwemo mauaji ya raia yanayofanywa na vikosi vya Marekani chini ya mwavuli wa shirika la kijeshi la NATO yakiendelea kushuhudiwa nchini humo…/