UNICEF: Maelfu ya watoto wakimbizi Waafrika wameingia Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i23443-unicef_maelfu_ya_watoto_wakimbizi_waafrika_wameingia_ulaya
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF limesema watoto wapatao 25,800 waliwasili nchini Italia mwaka 2016 wakiwa peke yao kwa lengo la kusaka hifadhi barani Ulaya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 14, 2017 07:08 UTC
  • UNICEF: Maelfu ya watoto wakimbizi Waafrika wameingia Ulaya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF limesema watoto wapatao 25,800 waliwasili nchini Italia mwaka 2016 wakiwa peke yao kwa lengo la kusaka hifadhi barani Ulaya.

Katika taarifa, UNICEF imesema kiwango hicho ni ongezeko la zaidi ya maradufu ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo watoto 12,360 waliingia Ulaya kama wakimbizi.

Meneja mwandamizi wa masuala ya dharura UNICEF, Lucio Melandri amesema idadi kubwa yao wanatoka Eritrea, Misri, Gambia na Nigeria wengi wao wakiwa wavulana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 17.

Amesema watoto hao wako hatarini kukumbwa na ukatili, huku akitupia lawama mifumo ya sasa ya ulinzi wa watoto akisema inachukua muda mtoto mkimbizi kusajiliwa kuwa mkimbizi au mhamiaji.

Wahamiaji wakiingia Ulaya kwa njia ya bahari wakiwa na watoto

Ili kukabiliana na hali hiyo, UNICEF inatoa mapendekezo sita kukiwemo kuondoa utaratibu wa kuwaweka korokoroni watoto wanaosaka hifadhi, kuwapatia watoto huduma za elimu na afya bila kusahau kushughulikia vyanzo vinavyosababisha watoto kukimbia nchi zao na kusaka ukimbizi na uhamiaji.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi za Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IMO, katika miezi 10 ya kwanza ya mwaka  2016, karibu wahajiri haramu laki tatu na 43 elfu na 589 walikuwa wameshaingia barani Ulaya kwa njia ya bahari.