Mar 24, 2017 04:32 UTC
  • Mhusika wa shambulio la London atajwa; majeruhi mwengine afariki dunia

Polisi ya Uingereza imetangaza kuwa mtu aliyehusika na shambulio la Jumatano kwenye kitovu cha mji mkuu wa nchi hiyo, London ni Khalid Masood mwenye umri wa miaka 52 ambaye ni mzaliwa wa Uingereza.

Taarifa iliyotolewa na Polisi ya London imeeleza kuwa Masood hakuwa miongoni mwa watu wanaofuatiliwa hivi sasa kwa uchunguzi wala hakukuwa na taarifa za kiintelijinsia kuhusu nia yake ya kuweza kufanya shambulio la kigaidi.

Wakati huohuo Polisi ya Uingereza imetangaza kuwa majeruhi mwengine wa shambulio hilo la kigaidi ambaye ni mzee mwanaume mwenye umri wa miaka 75 alifariki dunia jana usiku hopitalini kutokana na majeraha makubwa aliyopata, na kuifanya idadi ya waliofariki kufikia watu watano. Taarifa hiyo imeongeza kuwa hali za majeruhi watano ni mbaya, huku majeruhi wawili wakiwa hatarini kupoteza maisha.

Majeruhi wakikimbizwa hospitalini

Katika tukio hilo la Jumatano Masood, aliendesha gari katika eneo la watembeaji wa miguu na kuwagonga watu kadhaa karibu na majengo ya Bunge la Uingereza kabla ya kuteremka garini na kumchoma kisu askari polisi aliyekuwa katika ulinzi wa majengo hayo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani shambulio la kigaidi la London sambamba na kutoa wito kwa nchi zote kuunda muungano wa kweli, jumuishi na wa kimataifa kwa ajili ya kupambana kwa dhati na ugaidi…/ 

 

 

Tags