Mar 27, 2017 07:50 UTC
  • Waendesha mashtaka Korea Kusini washinikiza kukamatwa rais aliyeuzuliwa

Waendesha mashtaka nchini Korea Kusini wametoa wito wa kutolewa waranti wa kukamatwa rais aliyeondolewa madarakani hivi karibuni wa nchi hiyo, Park Geun-hye.

Taarifa ya waendesha mashtaka wa nchi hiyo imesema kuwa, Guen-hye mwenye umri wa miaka 65 anapaswa kukamatwa kutokana na uzito wa mashtaka yanayomuandama, yakiwemo ya ufisadi, kuvujisha taarifa nyeti za serikali na utumiaji mbaya wa ofisi ya rais.

Hata hivyo taarifa hiyo haijafafanua iwapo tayari imeviandikia barua rasmi Vyombo vya Mahakama kuvitaka vitoe waranti wa kukamatwa Guen-hye.

Park kabla ya kuondolewa madarakani

Mapema mwezi huu, Mahakama ya Katiba ya Korea Kusini iliafiki uamuzi wa Bunge wa kumuondoa madarakani Park Geun-hye, ikisisitiza kuwa alikiuka sheria na kuvuruga demokrasia.

Rais huyo aliyeondolewa madarakani alihusishwa na kashfa ya ufisadi kutoka makampuni makubwa nchini humo kwa kushirikiana na rafiki yake mkubwa, Choi Soon-Sil. Wawili hao wanakabiliwa na shtaka la kuchukua hongo kutoka mashirika hayo.

Licha ya kukanusha kwamba amehusika na kashfa hiyo, lakini Park Geun-hye katika miezi ya hivi karibuni amekuwa akiliomba taifa radhi mara kwa mara kutokana na uzito wa kadhia hiyo iliyozusha maandamano dhidi yake.

Tags