Mar 31, 2017 14:42 UTC
  • Rais aliyeuzuliwa Korea Kusini akamatwa na kuzuiliwa na polisi

Rais aliyeondolewa madarakani hivi karibuni wa Korea Kusini, Park Geun-hye amekamatwa na polisi ya nchi hiyo kwa tuhuma za ufisadi na utumiaji mbaya wa madaraka.

Geun-hye amekamatwa na anazuiliwa na polisi baada ya mahakama moja katika mji mkuu Seul kuidhinisha waranti wa kukamatwa kwake kutokana na tuhuma zinazomundama.

Geun-hye alisafirishwa hadi kusini mwa mji wa Seul ambako anazuiliwa kwenye jela moja akisubiri kusikilizwa kwa kesi dhidi yake. 

Siku chache zilizopita, waendesha mashtaka nchini Korea Kusini walitoa wito wa kutolewa waranti wa kukamatwa Park Geun-hye, kutokana na kile walichokitaja kuwa uzito wa mashtaka yanayomuandama, yakiwemo ya ufisadi, kuvujisha taarifa nyeti za serikali na utumiaji mbaya wa ofisi ya rais. 

Rais wa Korea Kusini kabla ya kuondolewa madarakani

Mapema mwezi huu, Mahakama ya Katiba ya Korea Kusini iliafiki uamuzi wa Bunge wa kumuondoa madarakani Park Geun-hye, ikisisitiza kuwa alikiuka sheria na kuvuruga demokrasia.

Rais huyo aliyeondolewa madarakani anahusishwa na kashfa ya ufisadi kutoka makampuni makubwa nchini humo likiwemo shirika la simu za rununu la Samsung, akishirikiana na mpambe wake wa karibu Choi Soon-Sil. 

Park Geun-hye anaweza kuzuiliwa kwa zaidi ya siku 20 kabla ya kupandishwa kizimbani rasmi na huenda akahukumiwa kifungo cha hadi miaka 10 jela iwapo atapatikana na hatia ya kula mlungula.

 

Tags