Apr 02, 2017 03:30 UTC
  • Watu 6 wauawa katika ufyatuaji risasi Marekani

Watu sita wameuawa katika kipindi cha masaa machache yaliyopita katika vitendo mbali mbali vya ufyatulianaji risasi kote Marekani.

Vyombo vya habari nchini Marekani vimeripoti ufyatulianaji risasi katika majimbo ya Texas, Florida, Illinois, Tennessee, Michigan, Kansas, Indiana, Maryland na Pennsylvania ambapo kwa ujumla watu sita wameuawa na wengine zaidi ya 18 kujeruhiwa.

Tokea mwanzoni mwa mwaka huu wa 2017, nchini Marekani kumeripotiwa visa 13,154 vya ufyatulianaji risasi ambapo kwa ujumla watu waliouawa katika matukio hayo ni 3,254 huku wengine 6,353 wakijeruhiwa.

Serikali iliyopita ya Obama ilijaribu kudhibiti umiliki wa silaha lakini mashirika makubwa yanayotengeneza silaha nchini Marekani yalitumia ushawishi katika bunge la nchi hiyo na kuzuia sheria hiyo kupitishwa.

Utafiti uliofanyika mwaka jana ulifichua kuwa uhalifu na jinai za kutisha zimeongeza kwa kiasi kikubwa katika miji mikubwa ya Marekani.

Utafiti huo uliofanywa na shirika la Major Cities Chiefs Association ulionyesha kuwa, kuna mauaji 307 zaidi yaliyofanyika katika miji mikubwa nchini humo katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka  2016, ikilinganishwa na mauaji yaliyofanyika katika muda kama huo mwaka 2015.

Eneo la jinai Marekani

Hivi karibuni Rais Donald Trump wa Marekani alikiri kuwa uhalifu, machafuko, jinai na mashambulizi ya silaha yameongezeka nchini humo.

Trump alisema hayo kwenye hotuba yake kwa Baraza la Congress la Marekani na kutaka hatua kali zichukuliwe za kukabiliana na uhalifu wa kutumia silaha, jinai na umaskini nchini humo.

Silaha nchini Marekani zinauzwa kama bidhaa nyingine za kawaida madukani na jambo hilo limepelekea kuenea silaha mikononi mwa watu ambao hawasiti kuzitumia kila wanapokasirishwa na jambo.

Tags