Radiamali ya awali ya Russia kwa shambulio la Marekani nchini Syria
Shambulizi la makombora ya Marekani dhidi ya Syria, ambalo limetekelezwa kwa amri ya kwanza ya kijeshi ya Rais Donald Trump dhidi ya serikali ya kigeni, limekabiliwa na radiamali tofauti na hasa kutoka Russia.
Ikiwa ni radiamali yake ya kwanza kwa shambulio hilo ambalo imesema limefanyika kinyume na sheria za kimataifa, Kremlin imesitisha ushirikiano wake wa anga na Marekani nchini Syria na kusisitiza kuwa hueda shambulio hilo likaharibu zaidi ushirikiano wa pande mbili. Akifafanua zaidi suala hilo, Dmitry Peskov Msemaji wa Ikulu ya Kremlin ya Russia amesema kuwa Rais Vladmir Putin wa nchi hiyo ambaye analichukulia shambulio hilo kuwa limefanyika dhidi ya nchi huru na inayojitawala, limetekelezwa kwa ajili ya kufunika mauaji ya raia yanayofanyika nchini Iraq. Awali Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ilitaka kuitishwa haraka iwezekanavyo kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kujadili shambulio hilo la Marekani dhidi ya Syria, na wakati huohuo kueleza masikitiko yake makubwa kuhusu uchokozi huo ambao umefanywa dhidi ya nchi inayopambana na ugaidi.
Kwa hakika hatua ya hivi karibuni ya kijeshi ya Marekai dhidi ya Syria inaweza kuchambuliwa katika mitazamo miwili tofauti. Mtazamo wa kwanza ni kuwa huenda shambulio hilo lisikaririwe tena na kwamba limefanyika kama jibu la Marekani kwa kile inachodai kuwa ni kukiukwa mstari wake mwekundu kuhusiana na suala la matumizi ya silaha za kemikali. Kwa mtazamo huo tunaweza kusema kuwa shambulio hilo halitakaririwa tena na kwamba iwapo italazimu ni maneno makali tu ndiyo yatakayotumika dhidi ya serikali ya Damascus katika siku zijazo. Mtazamo wa pili ni kuwa shambulio lililofanyika leo alfajiri ni mwanzo tu wa mashambulio mengine yanayotazamiwa kufanywa na Marekani dhidi ya Syria.
Kwa kutilia maanani kwamba kuna askari na zana nyingi za kijeshi za Russia katika pembe tofauti za ardhi ya Syria, ikiwa ni katika fremu ya ushirikiano wa nchi hizo kwa ajili ya kuwaangamiza magaidi wanaopigana dhidi ya serikali halali ya Damascus kwa ushirikiano wa nchi za kigeni zikiongozwa na Marekani na Saudi Arabia, ni wazi kuwa viongozi wa Moscow watachukua hatua za kivitendo kwa ajili ya kukabiliana na mashambulio ya Marekani dhidi ya Syria. Katika hali hiyo tunapasa kusubiri kushuhudia mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu ukibadilika na kuwa mgogoro mkubwa zaidi wa kimataifa. Kimsingi ushirikiano wa kijeshi wa Russia na Syria ulianzishwa kwa ajili ya kulinda maslahi makubwa zaidi ya kistratijia ya Moscow katika eneo hilo. Katika hali ya hivi sasa lengo muhimu zaidi la Russia ni kuilinda Syria kama eneo pekee la kistratijia la ushawishi wa Russia katika eneo la Mashariki ya Kati na ukanda wa bahari ya Mediterania na wakati huohuo kutumiwa nchi hiyo kama njia pekee ya kuimarisha ushawishi wa kisiasa na kijeshi wa Moscow Mashariki ya Kati.
kwa kutilia maanani kwamba kituo cha kijeshi cha Russia katika bandari ya Tartus nchini Syria ndicho kituo pekee cha Russia nje ya mipaka ya nchi hiyo, ni wazi kuwa Russia iko tayari kulipa thamani yoyote ile kwa ajili ya kukilinda kituo hicho cha kijeshi ili kulinda na kudhibiti mienendo na harakati za vikosi vyake vya majini. Hii ni katika hali ambayo kwa kuanzisha kituo kingine cha anga katika eneo la Hamim katika mkoa wa Lathiqiya nchini Syria Russia imeandaa uwanja wa kusalia kijeshi nchini humo kwa muda mrefu. Kwa msingi huo ni wazi kuwa Russia itasimama mbele ya nchi za Magharibi na hasa Marekani ili kulinda maslahi yake nchini Syria. Suala hilo linapata nguvu zaidi kwa kutilia maanani kwamba Russia vilevile imesimama imara mbele ya nchi hizo mashariki mwa Ulaya ili kutetea maslahi yake.