Jeshi la Myanmar Labomoa Msikiti wa Kihistoria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27446-jeshi_la_myanmar_labomoa_msikiti_wa_kihistoria
Jeshi la Myanmar limetumia mabuldoza kuubomoa kikamilifu msikiti wa kihistoria katika mkoa wa Waislamu wa Rakhine nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 08, 2017 07:33 UTC
  • Jeshi la Myanmar Labomoa Msikiti wa Kihistoria

Jeshi la Myanmar limetumia mabuldoza kuubomoa kikamilifu msikiti wa kihistoria katika mkoa wa Waislamu wa Rakhine nchini humo.

Msikiti huo  ulijengwa zaidi ya miaka 200 iliyopita kabla ya Myanmar, ambayo zamani ikijulikana kama Burma, kukoloniwa na Muingereza. 

Msikiti huo uliobomolewa Aprili tatu ulikuwa katika kijiji cha Lawei Dek, katika mji wa Buthidaung katika jimbo lenye Waislamu wengi la Rakhine magharibi mwa Myanmar. Msikiti huo ulifungwa na watawala wa Myanmar katikati ya muongo wa 1990 wakati ulipoanza mkakati wa mauaji ya kimbari ya Waislamu nchini humo.

Jeshi la Myanmar limeubomoa msikiti huo baada ya kutekeleza jinai mbali mbali dhidi ya Waislamu ikiwa ni pamoja na kuwaua kiholela, kuwanajisi wanawake, kuteketeza nyumba na vijiji, na kutekeleza njama ya mauaji ya kimbari. Hakuna shaka kuwa hatua ya kubomolewa msikiti huo ni katika fremu ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu na imetekelezwa kwa idhini ya serikali ya Myanmar.

Wanajeshi wa Myanmar

Hayo yanajiri wakati ambao Aung San Suu Kyi kiongozi wa ngazi za juu  na Waziri wa Mambo ya Nje ya Myanmar  kukanusha kuwepo mauaji ya kimbari ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini humo pamoja na kuwa taasisi za kimataifa zikiwemo za Umoja wa Mataifa zimechapisha ripoti zinazoonyesha kuna njama za makusudi za kuwaangamiza Waislamu kwa umati nchini humo.

Hatua ya jeshi la Myanmar kulenga na kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu hasa kubomoa msikiti wa kihistoria ni jambo linaloonyesha kuwa, kimya mutlaki cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mbele ya jinai za kivita na mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu katika jimbo la Rakhine  ni chanzo cha kuongezeka na kuendelea ukandamizaji wa Waislamu nchini Myanmar.

Kuna uwezekano mkubwa kuwa, Jeshi la Myanmar limebomoa msikiti wa kihistoria wa Waislamu ili kufuta historia ya kuwepo kwao nchini humo. Hilo linafanyika katika fremu ya madai ya urongo ya wakuu wa Myanmar kuwa, Waislamu wa kabila la Rohingya ni wahajiri kutoka Bangladesh wasio na mizizi ya kihistoria Myanmar.

Hii ni katika hali ambayo Waislamu wana historia ya karne nyingi nchini Myanmar na hata ustaarabu na utamaduni wao umeweza kuwa na taathiria katika nchi hiyo. Waislamu wamekuwa na nafasi muhimu sana na yenye taathira katika sekta za elimu, utamaduni na uchumi wa Myanmar.

Waislamu wa Myanmar wakiwa katika kambi ya wakimbizi

Kitendo cha Jeshi la Myanmar kuharibu msikiti wa kihistoria katika mji wa Buthidaung ni jambo linaloashiria kuanza uhasama mpya wa jeshi hilo wenye lengo la kufuta kikamilifu athari za kihistoria na matukufu ya Waislamu nchini humo.

Baadhi ya weledi wa mambo wanaamini kuwa, kushadidi ukatili wa watawala wa Myanmar dhidi ya Waislamu na matukufu yao ni natija ya sera za chuki dhidi ya Waislamu katika nchi za Magharibi hasa Marekani. Wakuu wa Myanmar wamekuwa wakiiga bila kuogopa yanayojiri katika nchi hizo za Magharibi. Ni kwa msingi huo ndio tokea mwezi Oktoba mwaka 2016 kumeshuhudiwa wimbi jipya la mauaji na ukandamizaji wa Waislamu nchini Myanmar.

Kwa maelezo hayo tunaweza kusema kuwa, nchi za Magharibi na hasa Marekani ni washirika wa jinai dhidi ya Waislamu wa kabila la  Rohingya nchini Myanmar, kwani kimya cha nchi hizo zinazodai kutetea haki za binaadamu ndicho chanzo cha kupata kiburi na ujasiri wakuu wa Myanmar katika utekelezaji wa njama zao za mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu.