Wamarekani waandamana kupinga mashambulizi ya nchi hiyo dhidi ya Syria
Wananchi wa Marekani wamefanya maandamano katika miji mbalimbali ya nchi hiyo wakipinga sera za kupenda vita na ubabe za serikali ya Rais mpya wa nchi hiyo, Donald Trump.
Waandamanaji katika miji ya Washington, New York, Los Angeles na Philadelphia walikuwa wakipiga nara za kupinga mashambulizi ya jeshi la Marekani dhidi ya Syria na kuwatetea raia wa nchi hiyo.
Ripoti zinasema maandamano hayo yamekabiliwa na ukandamizaji mkuwa wa polisi ya Marekani ambao walionekana kwa wingi katika miji hiyo. Waandamani hao wa Marekani wamesisitiza kuwa, mashambulizi dhidi ya Syria si utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo na kwamba badala yake yatazidisha hali mbaya.
Inatazamiwa kuwa kutashuhudiwa maandamano makubwa zaidi katika miji 50 ya Marekani kupinga siasa za kupenda vita za serikali ya nchi hiyo.
Mashambulizi ya makombora yaliyofanywa usiku wa kuamkia jana na jeshi la Marekani dhidi ya kituo cha anga cha Syria katika mkoa wa Homs yameua raia 9 wakiwemo watoto 4 na kujeruhi wengine 7. Mashambulizi hayo yamefanyika bila ya ruhusa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wala Kongresi ya Marekani.
Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov amesema kuwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya Syria yamefanyika kinyume cha sheria za kimataifa na kwamba hayawezi kukubalika. Lavrov amesema mashambulizi hayo yatazidisha mgogoro nchini Syria.