Apr 12, 2017 07:11 UTC
  • Amnesty yasema mashambulizi ya Marekani dhidi ya Syria ni ya jazba

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limelaani vikali hatua ya Marekani ya kukishambulia kituo cha kijeshi cha Syria kwa makombora na kusisitiza kuwa 'mashambulizi hayo ya jazba' sio njia mbadala ya kufanyika uchunguzi wa kina juu ya mashambulizi ya silaha za kemikali katika eneo la Khan Sheikhoun.

Katibu Mkuu wa Amnesty International, Salil Shetty amesema kitendo cha Marekani kuishambulia Syria katu hakiwezi kuipatia ufumbuzi kadhia iliyopo huku akizikashifu nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuingiza siasa katika mgogoro wa Syria.

Kadhalika Shetty amesisitiza kuwa, hatua kama hiyo ya Marekani kuishambulia Syria ni ishara na ithibati kuwa, jitihada za kimataifa za kutaka kutekelezwa haki za binadamu duniani ziko katika kinamasi. 

Makombora ya Tomahawk ya Marekani yaliyolenga Syria

Usiku wa kuamkia Ijumaa, Marekani ilivurumisha makombora 59  kutokea katika meli zake mbili za kivita katika bahari ya Mediterania na kukishambulia kituo cha jeshi la anga la Syria katika eneo la Shayrat katika mkoa wa Homs na kuuwa watu tisa wakiwemo watoto wanne na kujeruhi wengine kadhaa. 

Rais Donald Trump wa Marekai aliagiza kutekelezwa mashambulizi hayo, kwa kisingizio bandia kuwa serikali ya Rais Bashar al-Assad ya Syria ilitumia silaha za kemikali dhidi ya raia wa nchi hiyo, suala ambalo lilikanushwa vikali na serikali ya Damascus.

Hii ni katika hali ambayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Javad Zarif ametilia mkazo udharura wa kuundwa tume ya kimataifa ya kufanya uchunguzi kuhusu mashambulizi hayo ya silaha za kemikali Jumanne ya wiki jana, ambapo makumi ya watu waliuawa. 

Tags