Mgogoro wa kutoaminiana katika uhusiano wa Moscow na Washington
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27734-mgogoro_wa_kutoaminiana_katika_uhusiano_wa_moscow_na_washington
Mazungumzo ya kwanza kati ya Rais wa Russia na Rex Tillerson Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani hayajaandaa uwezekano wa kujenga hali ya kuaminiana kati ya Moscow na Washington.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Apr 13, 2017 22:11 UTC
  • Mgogoro wa kutoaminiana katika uhusiano wa Moscow na Washington

Mazungumzo ya kwanza kati ya Rais wa Russia na Rex Tillerson Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani hayajaandaa uwezekano wa kujenga hali ya kuaminiana kati ya Moscow na Washington.

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema baada ya mazungumzo na Rex Tillerson kuwa kiwango cha maaminiano kati ya Marekani na Russia wakati wa utawala wa Rais Donald Trump kimekuwa kibaya. Kabla ya hapo pia Rex Tillerson alitoa maoni sawa na hayo akisema kuwa, uhusiano wa Marekani na Russia hivi sasa ni wa kiwango cha chini na kwamba maaminiano kati ya nchi mbili hizo yamekuwa dhaifu. Bila shaka viongozi wote wawili wa Russia na Marekani wameeleza matarajio yao ya kuboreka uhusiaino huu wa sasa ambao ni tete sana na uliovurugika. Pamoja na hayo yote, pande mbili hizo zimeshindwa pia kuwa na maelewano kuhusu kadhia ya Syria.

Rais Putin wa Russia katika mazungumzo na Rex Tillerson Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani 

Hakuna shaka kuwa kuwepo hali ya kutoaminiana kati ya Moscow na Washington hakukomei tu katika mgogoro wa Syria na hali ya kisiasa ya baadaye ya nchi hiyo. Tangu miaka 100 iliyopita hadi sasa, Moscow na Washington hazijakuwa zikiaminiana kwa kiwango kinachotarajiwa. Hata katika zama za mapambano ya pamoja dhidi ya Ufashisti wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, Warussia  Wakomonisti na Mabepari wa Kimarekani walikuwa wakitazamana kwa jicho la shaka. Kumalizika vita dhidi ya Ufashisti kuliwapelekea waitifaki hao wawili katika Vita vya Pili vya Dunia kugeuka na kuwa mahasimu katika kipindi cha vita baridi. Hali hiyo ya kutoamianiana kati ya nchi mbili hizo mwishoni mwa vita baridi, kuliifanya dunia ikaribie kupigana vita vya nyuklia kutokana na mgogoro wa makombora uliokuwa ukiikabili Cuba; na kusababisha pia vita vingi vya kieneo katika pembe mbalimbali za dunia. Kumalizika vita baridi na kusambaratika Umoja wa Kisovieti pia hakukuleta mabadiliko katika hali ya kutoaminiana ambayo imekuwepo kwa muda mrefu kati ya Warussia na Wamarekani. Kama wanavyosema viongozi wa nchi mbili hizo,  uhusiano kati ya Moscow na Washington hivi sasa umeharibika zaidi kulinganisha na huko nyuma. 

Chimbuko la kutoaminiana huko ni mitazamo waliyonayo wasomi na wananchi wa nchi mbili hizo. Katika kipindi chote cha historia, Warusi wamekuwa wakizishuku nchi za Magharibi ikiwemo Wamarekani; huku wakiamini kuwa nchi hizo zinafanya juhudi za kuidhoofisha Russia na kuifanya iwe tegemezi. Tangu zama za Peter the Great katika karne ya 17 hadi Vladimir Putin katika karne ya 21, watawala wote wa Russia, iwe ni Watazari, Wakomonisti au Wazalendo wamekuwa wakibainisha wazi  wasiwasi walionao kuhusu kupenda kujitanua nchi za Magharibi na kupuuza maslahi ya taifa la Russia. Kuna kila dalili na sababu ya kuthibitisha wasiwasi huu. Kwa mfano katika miaka ya hivi karibuni ambapo kumezuka mchuano wa kiadiolojia kati ya Wakomonisti na Mabepari,  nchi za Magharibi zingali zinatumia nyenzo kama za kupanua Muungano wa Kijeshi wa nchi hizo (NATO) kuelekea katika mipaka ya Russia na kuyapora maeneo yenye ushawishi ya Moscow huko Ulaya Mashariki, Asia ya Magharibi na Kaskazini mwa Afrika kwa lengo la kuibana na kuidhibiti Russia. Si hayo tu, bali kila hatua ya kulegeza msimamo au kufikia muafaka ambayo imekuwa ikichukuliwa na Russia baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti pia imekuwa ikikabiliwa na kusonga  mbele nchi za Magharibi katika medani nyingine. Mashinikizo hayo yote yaliendelea kiasi kwamba Magharibi ilianzisha vita vya umwagaji damu huko Chechniya na kufanya kila iwezalo ili kuasisi mapinduzi ya rangi ya njano huko Russia. 

Sehemu ya maafa katika Vita vya Kwanza vya Chechniya 

Hata hivyo nchi za Magharibi chini ya uongozi wa Marekani pia zinatoa visingizio vinavyozifanya ziendeleze siasa zao hizo dhidi ya Russia. Zinadai kuwa wazalendo wa Russia wanafanya jitihada za kustafidi na hali ya mgogoro duniani kwa maslahi yao na hivyo kuasisi mfumo mpya wa utawala duniani. Nchi za Magharibi zinaona kuwa kutekelezwa mashambulizi dhidi ya  Georgia, kuvamiwa Crimea, kuibua machafuko huko Ulaya Mashariki, kuibua tatizo la nishati barani Ulaya, hatua ya Russia ya kujiiimarisha nchini  Afghanistan na kuunga mkono mfumo wa kisiasa huko Syria,  ni sehemu ya hatua za Russia za kupenda  kujitanua kisiasa, kiusalama na kiuchumi.

Hivi sasa ambapo kuna anga ya kutoaminiana kikamilifu kati ya Marekani na Russia, nchi mbili hizo zinajaribu kujidhihirisha kuwa juu ya nyingine ili kufikia muafaka.  Mwenendo huo ambao ulipamba moto wakati wa utawala wa Rais Barack Obama umeacha athari kubwa hivi sasa  baada ya kuingia madarakani serikali mpya na mrengo unaopenda vita huko Marekani. Katika mazingira kama hayo, ni wazi kuwa hatua yoyote ya kichokozi kama ile ya mashambulizi ya makombora iliyotekelezwa na Marekani katika kituo cha kijeshi huko Syria  inaweza kuanzisha vita kati ya nchi mbili hizo.