Wabunge Marekani wapanga kumzuia Trump kuiuzia Saudia silaha
https://parstoday.ir/sw/news/world-i29610-wabunge_marekani_wapanga_kumzuia_trump_kuiuzia_saudia_silaha
Wabunge kadhaa nchini Marekani wanapanga kuanzisha sheria ya kumzuia Rais Donald Trump kuiuzia Saudia baadhi ya silaha.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
May 26, 2017 03:04 UTC
  • Wabunge Marekani  wapanga kumzuia Trump kuiuzia Saudia silaha

Wabunge kadhaa nchini Marekani wanapanga kuanzisha sheria ya kumzuia Rais Donald Trump kuiuzia Saudia baadhi ya silaha.

Seneta wa chama cha Trump cha Republican Rand Paul na maseneta wa chama cha Democrat Chris Murphy na Al Franken wamewasilisha muswada wa siku ya Alhamisi kuilaizmu serikali kufuta dola milioni 500 kati ya dola bilioni 110 za mapatano hayo ya awali ya silaha.

Paul anasema anapinga mapatano hayo ya silaha yaliyotiwa saini siku ya Jumapili baina ya Trump na Mfalme Salman wa Saudia mjini Riyadh kwa sababu Saudi Arabia inaunga mkono makundi ya kigaidi na inaweza kutumia silaha hizo katika vita vyake dhidi ya Yemen. Amesema Saudia inatumia mbinu chafu katika vita dhidi ya Yemen.

Silaha za Marekani

Aidha seneta huyo mashuhuri amesema Saudia ina rekodi mbaya ya haki za binadamu. Seneta Paul amesema Trump anataka kuimarisha uuzaji wa silaha za Marekani duniani kama njia ya kubuni nafasi za ajira nchini humo.

Moja ya matukio muhimu zaidi ya safari ya Trump mjini Riyadh ni kutiwa saini mkataba wa ununuzi silaha zenye thamani ya dola bilioni 350 ambapo awamu ya kwanza ya mauzo hayo ni ya dola bilioni 110.