Umoja wa Mataifa kuanzisha ofisi ya kupambana na ugaidi
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, utaanzisha ofisi maalumu ya kupambana na ugaidi ikiwa ni katika juhudi za umoja huo za mikakati mipya ya kukabiliana na vitendo vya ugaidi ulimwenguni ambavyo vinazidi kuongezeka siku baada ya siku.
Tayari Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kuanzisha ofisi ya kupambana na ugaidi, ili kuratibu juhudi zinazofanywa na mashirika ya Umoja wa Mataifa katika mapambano dhidi ya ugaidi.
Hatua hiyo imetajwa kuwa ni mageuzi makubwa ya kwanza ya kitaasisi yaliyofanywa katika Umoja wa Mataifa tangu Bw. Antonio Guterres achukue nafasi hiyo ya Ukatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akimrithi Ban Ki-moon.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jana lilipasisha pendekezo la kuanzishwa ofisi ya kupambana na ugaidi lililowasilishwa na Antonio Guterres.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia msemaji wake, amekaribisha kupitishwa kwa azimio hilo, na kusema kuwa, anatarajia kuwa mageuzi hayo yanaweza kuhimiza juhudi za Umoja wa Mataifa katika kuzuia migogoro na kuhimiza maendeleo na amani ya kudumu.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, vitendo vya ugaidi vimekuwa vikishamiri siku baada ya siku katika maeneo mbalimbali duniani na hivyo kuhatarisha usalama na amani.
Baadhi ya madola makubwa ulimwenguni yanakosolewa kutokana na siasa zao za kindumakuwili katika suala zima la kupambana na ugaidi huku baadhi yao yakiyaunga mkono makundi ya kikaidi kama Daesh na mengineyo kwa kuyapatia fedha na silaha. Undumakuwili huo unatajwa kuwa kikwazo katika vita vya kweli dhidi ya ugaidi.