Pyongyang: Maafisa Usalama wa Marekani wamewadhalilisha wanadiplomasia wetu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i30704-pyongyang_maafisa_usalama_wa_marekani_wamewadhalilisha_wanadiplomasia_wetu
Serikali ya Korea Kaskazini imetangaza kuwa, maafisa usalama wa Marekani wamewavunjia heshima wanadiplomasia wa nchi hiyo kwa kuwasimamisha na kupekua mabegi yao kwa nguvu katika uwanja wa ndege wa John F. Kennedy nchini Marekani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 20, 2017 02:32 UTC
  • Pyongyang: Maafisa Usalama wa Marekani wamewadhalilisha wanadiplomasia wetu

Serikali ya Korea Kaskazini imetangaza kuwa, maafisa usalama wa Marekani wamewavunjia heshima wanadiplomasia wa nchi hiyo kwa kuwasimamisha na kupekua mabegi yao kwa nguvu katika uwanja wa ndege wa John F. Kennedy nchini Marekani.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini sambamba na kulaani kitendo hicho, imetangaza kwamba, wanadiplomasia wa nchi hiyo walikumbwa na adha hiyo wakati walipoenda kushiriki kongamano la kimataifa mjini New York, Marekani ambapo wakati wakijiandaa kurudi nchini kwao walisimamishwa na maafisa usalama wa Marekani katika uwanja wa ndege na kuanza kuvunjiwa heshima ikiwa ni pamoja na kupekuliwa wao na mabegi yao kwa nguvu.

Mabegi ya wanadiplomasia hao wa Korea Kaskazini

 

Nalo Shirika la Habari la Korea Kaskazini limetangaza kuwa, kufuatia kitendo hicho kilichotajwa kuwa cha kichochezi, Pyongyang imeitaka serikali ya Marekani kutoa maelezo ya kina kuhusiana na hatua hiyo inayokinzana na sheria za kimataifa zinazowalinda wanadiplomasia.

Kwa mujibu wa shirika hilo, wakati wanadiplomasia hao wa Korea Kaskazini walipoonyesha upinzani dhidi ya unyanyasaji huo maafisa usalama wa uwanja wa ndege wa Marekani walitumia nguvu kuwanyang'anya mabegi na mali zao nyingine.

Uwanja wa ndege wa John F. Kennedy nchini Marekani

Pyongyang imeitaka jamii ya kimataifa kupanga eneo lingine kwa ajili ya kuendeshea mikutano ya kimataifa sambamba na kuimarisha usalama.