Maandamano yafanyika Marekani baada ya kuuawa binti Muislamu
Habari ya kuuawa msichana mmoja wa Kiislamu nchini Marekani katika shambulizi lililofanywa na mtu mwenye chuki dhidi ya dini ya Uislamu katika jimbo la Virginia imezusha malalamiko na maandamano nchini humo.
Mbali na maandamano ya kulaani mauaji hayo kufanyika katika sehemu mbalimbali nchini humo, Waislamu katika mitandao ya kijamii wamekosoa vikali kitendo hicho cha kuuawa binti huyo aliyekuwa na umri wa miaka 17 kwa misingi ya dini yake.
Binti huyo Muislamu kwa jina la Nabra Hassanen, aliuawa Jumapili iliyopita baada ya kutoka msikitini katika jimbo hilo ambapo alitekwa nyara na kupigwa na mtu mwenye chuki za kidini jimboni hapo.
Polisi imetangaza kuwa imemtia mbaroni na kumfungulia mashtaka kijana huyo aliyejulikana kwa jina la Darwin Martinez Torres mwenye umri wa miaka 22.
Wakati huo huo, baba wa Nabras, Mohmoud Hassanen amekanusha vikali madai ya polisi ya Marekani kwamba bintiye aliuawa katika 'ajali mbaya ya barabarani' na kusisitiza kuwa, aliuawa kwa kuwa ni Muislamu.
Hii sio mara ya kwanza kwa mfuasi wa dini tukufu ya Kiislamu kuuawa nchini Marekani kutokana na kushadidi chuki dhidi ya Waislamu na wahajiri.
Kwa mujibu wa Baraza la Mahusiano ya Kiislamu nchini Marekani, mashambulizi yanayowalenga Waislamu nchini humo yaliongezeka kwa karibu asilimia 57 mwaka jana 2016 kutoka kesi 1409 mwaka 2015 na kufikia 2213, ongezeko linaloaminika kutokana na matamshi ya chuki ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo dhidi ya Waislamu na wahajiri.