Pyongyang: Vitisho vya Marekani haviwezi kutuzuia kujiimarisha kwa nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i31114-pyongyang_vitisho_vya_marekani_haviwezi_kutuzuia_kujiimarisha_kwa_nyuklia
Balozi wa Korea Kaskazini katika Umoja wa Mataifa ameiambia Marekani na washirika wake kwamba, Pyongyang itaendelea kujiimarisha kwa silaha za nyuklia na haitojali vikwazo, mashinikizo na vitisho vya Washington na washirika wake vya kuishambulia kijeshi nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 29, 2017 14:19 UTC
  • Pyongyang: Vitisho vya Marekani haviwezi kutuzuia kujiimarisha kwa nyuklia

Balozi wa Korea Kaskazini katika Umoja wa Mataifa ameiambia Marekani na washirika wake kwamba, Pyongyang itaendelea kujiimarisha kwa silaha za nyuklia na haitojali vikwazo, mashinikizo na vitisho vya Washington na washirika wake vya kuishambulia kijeshi nchi hiyo.

Kim In Ryong, balozi wa Korea Kaskazini na mwakilishi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa ameyasema hayo mbele ya Baraza la Usalama la umoja huo kufuatia mwendelezo wa siasa za uhasama za Marekani na maneva mtawalia ya kijeshi yanayofanywa na nchi hiyo kwa kushirikiana na Korea Kusini katika Peninsula ya Korea.

Kim In Ryong balozi wa Korea Kaskazini na mwakilishi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa

Amesema kuwa, tofauti na huko nyuma, hivi sasa Peninsula ya Korea inakabiliwa na vita vya nyuklia, hivyo, Pyongyang itaendelea kujiimarisha kwa silaha za nyuklia ili kwenda sambamba na tishio la silaha hizo. Mwakilishi wa Korea Kaskazini katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, hakuna hatua yoyote ile ya Marekani ikiwemo ya kuweka ngao ya makombora ya kisasa aina ya THAAD nchini Korea Kusini na wala vikwazo vipya dhidi ya Pyongyang, inayoweza kuizuia nchi yake kujiimarisha kwa silaha za nyuklia.

Moja ya silaha za nyuklia za Korea Kaskazini

Hadi sasa Peninsula ya Korea imeendelea kushuhudia harakati nyingi za kijeshi kutokana na siasa za uhasama za Marekani kwa kushirikiana na washirika wake, yaani Korea Kusini na Japan. Katika hatua nyingine, serikali ya Pyongyang imetaka kunyongwa rais wa zamani wa Korea Kusini, Bi Park Geun-hye na mkuu wa zamani wa idara ya usalama wa taifa wa nchi hiyo, Lee Byung-ho kwa kile ilichokisema kuwa, ni kupanga njama chafu za kutaka kumuua Kim Jong Un, kiongozi wa Korea Kaskazini.

Bi Park Geun-hye, rais wa zamani wa Korea Kusini akiwa chini ya ulinzi

Taarifa iliyotolewa na viongozi wa Korea Kaskazini sambamba na kuashiria njama hizo za kutaka kumuua kiongozi wa nchi hiyo mwaka 2015, imeitaka serikali ya Seoul kuwakabidhi kwa Pyongyang Bi Park Geun-hye na Lee Byung-ho ili wahukumiwe huko. Hii ni katika hali ambayo idara ya usalama wa taifa ya Korea Kusini imesema kuwa madai hayo ya Korea Kaskazini hayana msingi.