Ripoti mpya ya SIPRI kuhusiana na kuongezeka silaha za nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i31354-ripoti_mpya_ya_sipri_kuhusiana_na_kuongezeka_silaha_za_nyuklia
Ripoti mpya ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) inaonyesha kuwa, mwenendo wa uwekezaji katika masuala ya silaha za nyuklia kwa ajili ya kuzifanya silaha hizo kuwa za kisasa umeongezeka duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 05, 2017 03:38 UTC
  • Ripoti mpya ya SIPRI kuhusiana na kuongezeka silaha za nyuklia

Ripoti mpya ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) inaonyesha kuwa, mwenendo wa uwekezaji katika masuala ya silaha za nyuklia kwa ajili ya kuzifanya silaha hizo kuwa za kisasa umeongezeka duniani.

Licha ya kuwa katika mwaka uliopita wa 2016 idadi ya silaha za nyuklia duniani ilipungua, lakini mwenendo wa uwekezaji wenye lengo la kuziboresha na kuzifanya silaha hizo zilizozalishwa kuwa za kisasa zaidi umeonekana ukiongezeka katika maeneo mbalimbali duniani.

Kwa sasa Marekani, Russia, Uingereza, Ufaransa, China, India, Pakistan, Korea Kaskazini na utawala wa Kizayuni wa Israel ndizo zenye kumiliki silaha za nyuklia ambapo mpaka kufikia mwaka huu, tawala hizo zinamiliki jumla ya vichwa 14,395 vya nyuklia. Kiwango hicho ni pungufu kidogo ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake ambapo tawala hizo kwa pamoja zilikuwa zikimiliki vichwa 15,395 vya nyuklia.

Silaha za nyuklia za Marekani

Kupungua kwa kiwango fulani idadi ya vichwa hivyo vya nyuklia, ni natija ya makubaliano ya nguvu mbili kubwa za nyuklia yaani Marekani na Russia katika fremu ya mkataba wa Start.

Madola hayo mawili yanamiliki asilimia 93 ya silaha zote za atomiki duniani.

Pamoja na hayo, kungali kuna mashindano makubwa baina ya madola makubwa ya kuziboresha na kuzifanya kuwa za kisasa zaidi silaha zao za nyuklia. Kannon Kile, mmoja wa wataalamu wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) ametangaza kuwa, licha ya kupigwa hatua katika mazungumzo ya kimataifa kuhusiana na kupiga marufuku silaha za nyuklia, kila moja kati ya madola 9 yenye kumiliki nguvu za nyuklia ulimwenguni limetangaza kuwa, imepanua mfumo wake wa kubeba makombora.

Kimsingi ni kuwa, pamoja na kuweko hatua za kimataifa za kupunguzwa silaha za nyuklia hususan mkataba wa kuzuia uzalishaji na usambazaji wa silaha za nyuklia NPT ambao ulipasishwa katika fremu ya kupunguza na hatimaye kutokomeza kabisa silaha hizo, lakini madola makubwa ya nyuklia yaani nchi tano wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, zingali zimeng'ang'ania msimamo wao wa kuendelea kuwa na silaha zao hizo.

Makombora ya nyuklia ya Korea Kaskazini

Nchi hizo zikitumia kisingizio cha mwenendo wa kuzifanya kuwa mpya silaha zao za nyuklia zimetenga bajeti kubwa katika uwanja huo. Inaelezwa kuwa, Russia imekusudia kuwa, hadi kufikia mwaka 2020 iwe imeweza kuifanya asilimia 70 ya silaha zake za nyuklia kuwa mpya na za kisasa zaidi.

Pamoja na hayo Marekani ina mipango mipana zaidi katika uga huo ikilinganishwa na Russia ambapo katika kipindi cha miaka kumi imepanga kutumia dola bilioni 350 katika uwanja huo. 

Kuhusiana na hilo, Hans Kristensen, mtaalamu mwingine wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) anasema kuwa, serikali mpya ya Marekani inaendeleza mpango wa kuzifanya kuwa za kisasa silaha za nyuklia za nchi hiyo, uliokuwa umeanzishwa na Rais aliyetangulia wa nchi hiyo Barack Obama.

Yukia Amano Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.

Tukiachana na Marekani na Russia, nchi nyingine zenye kumiliki silaha za nyuklia ambazo zinatambuliwa rasmi kama wanachama wa klabu ya nyuklia yaani Ufaransa, Uingereza na China nazo zimo katika prikapirika za kutengeneza silaha na mifumo mipya ya kurushia mabomu ya nyuklia au zimeazimia kufanya hivyo.

Hakuna nchi hata moja kati ya hizo inayofikiria au yenye mpango wa kupunguza silaha zake za nyuklia au kuandaa jedwali maalumu kwa ajili ya kutokomeza silaha hizo.

Wakati huo huo, nchi nyingine nazo ambazo katika miaka ya hivi karibuni zilijiunga katika klabu ya nyuklia, daima zimekuwa mbioni kuongeza silaha hizo na kuboresha zaidi kiwango chake.

Katika mazingira kama haya, tishio linalotokana na silaha za nyuklia linapata maana halisi hasa kutokana na kuweko maelfu ya silaha za nyuklia katika maghala ya silaha ya madola makubwa na kuweko baadhi ya nchi nyingine ambazo katika miongo ya hivi karibuni zimefanikiwa kutengeneza silaha hizi hatari na kuwa miongoni mwa madola yanayomiliki silaha za nyuklia ulimwenguni.