Umoja wa Mataifa walaani mauaji dhidi ya Waislamu wa Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i33622-umoja_wa_mataifa_walaani_mauaji_dhidi_ya_waislamu_wa_myanmar
Umoja wa Mataifa umelaani vikali mauaji na vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 26, 2017 03:53 UTC
  • Umoja wa Mataifa walaani mauaji dhidi ya Waislamu wa Myanmar

Umoja wa Mataifa umelaani vikali mauaji na vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa jana Ijumaa imekemea na kukosoa vikali mashambulio ya kuratibiwa ya vikosi vya usalama vya Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya katika mkoa wa Rakhine ulioko magharibi mwa nchi hiyo. 

Renata Lok-Dessallien, Mratibu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Myanmar ameonyesha wasiwasi mkubwa alionao kutokana na hali ya usalama katika jimbo la Rakhine na kusema kuwa, pande zote mbili zinapaswa kujiepusha na vitendo vya utumiaji mabavu na wakati huo huo kudumishwa ulinzi kwa raia.

Radiamali hiyo ya Umoja wa Mataifa imekuja masaa machache baada ya Waislamu 35 kuuawa katika mapigano yaliyozuka usiku wa kuamkia jana nchini Myanmar katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa nchi hiyo.

Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar wakikimbia makazi yao kukwepa mashambulio ya mabudha 

Mapema mwezi huu Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) iliitaka serikali ya Myanmar iheshimu haki za Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo ambao wanakandamizwa na vikosi vya usalama na kuhujumiwa na Mabudha wenye misimamo mikali. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Waislamu wa kabila la Rohingya ni jamii ya wachache inayodhulumiwa na kunyongeshwa zaidi duniani. 

Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Bangladesh, Thailand, Malaysia na Indonesia wakikimbia mashambulio ya Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada wanaoungwa mkono na serikali.