Waislamu 300,000 watazamiwa kukimbia mauaji nchini Myanmar
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa Waislamu zaidi ya 300,000 wanatazamiwa kukimbia mauaji na dhulma wanazotendewa nchini Myanmar na kuelekea katika nchi jirani ya Bangladesh.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanakadiria kuwa katika kipindi cha wiki mbili sasa, Waislamu 146,000 wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar tayari wameshafika katika eneo la mpakani la Bangladesh la Cox's Bazaar. Wanasema ni vigumu kukadiria kikamilifu idadi ya wakimbizi kwa sababu oparesheni za jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu zingali zinaendelea. Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP nchini Bangladesh Dipayan Bhattacharyya amesema wakimbizi wengi wanakabiliwa na lishe duni kwani kwa muda wa mwezi mmoja hawajaweza kupata chakula cha kutosha walipokuwa nchini Myanmar.
Taarifa zinasema zaidi ya Waislamu 3,000 wameuawa kwa umati tokea Agosti 25 wakati wa kuanza wimbi jipya la ukatili wa jeshi katika jimbo lenye Waislamu wengi la Rakhine nchini Myanmar.
Pamoja na kuwepo ushahidi wa mauaji ya kimbari ya Waislamu na hata baada ya kuzuiwa mashirika ya Umoja wa Mataifa kuingia katika jimbo la Waislamu la Rakhine nchini Myanmar, jamii ya kimataifa haijachukua hatua zozote za maana na imefumbia macho ukandamizaji huo wa Waislamu. Hali kadhalika vyombo vya habari vya Magharibi pia kwa ujumla vimepuuza mauaji ya Waislamu nchini Myanmar huku baadhi vikidai kuwa eti waliouawa ni magaidi.
Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za jirani kutokana na mashambulio ya Mabuddha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.