Dec 04, 2017 14:50 UTC
  • Mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji azma ya kimataifa

Kongamano la Kimataifa la Kupambana na Dawa za Kulevya limenaza leo mjini Moscow, Russia kwa kushirikisha maspika wa mabunge ya nchi zaidi ya 40.

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, Ali Larijani anashiriki katika kongamano hilo akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa Iran.

Biashara ya dawa za kulevya ina taathira hasi kieneo na kimataifa na sasa ni tishio kubwa kwa dunia. Kwa msingi huo kupambana na uovu huu hatari, sawa na mapambano dhidi ya ugaidi ni jambo linalohitajia azma na irada ya kimataifa.

Takwimu na ripoti zinaonyesha kuwa nchi za Ulaya na Amerika Kaskazini ndiyo masoko makubwa zaidi ya dawa za kulevya zinazokuzwa katika mashamba ya nchini Afghanistan. Afiuni hiyo ya Afghanistan husafirishwa katika masoko ya Ulaya na Marekani kupitia nchi jirani.

Ahmad Javid Qaim, Naibu Waziri wa Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Afghanistan anasema: "Nchi zinazopakana na Afghanistan zinapaswa kushirikiana katika vita dhidi ya mihadarati na ziwe na mapatano jumla kuhusu namna ya kukabiliana na dawa za kulevya."

Askari wa Iran akiwa analinda doria mpakani na Afghansitan

Jamuri ya Kiislamu ya Iran iko katika mstari wa mbele wa kupambana na dawa za kulevya duniani  na hadi sasa askari wake zaidi ya 3,500 wameuawa shahidi katika vita vya kupambana na wafanyabishara haramu wa kuuza au kusafirisha dawa za kulevya. Kutokana na kupakana na Afghanistan ambayo ni mzalishaji mkubwa wa afiuni duniani, wafanyabiashara haramu wa dawa za kulevya hujaribu mara kwa mara kupitishia mihadarati yao humu nchini.

Mwaka 2016, vikosi vya usalama Iran vilifanikiwa kutekeleza oparesheni 2,300 na kuweza kunasa kilo 681,576 za aina mbali mbali za mihadarati. Ikilinganishwa na mwaka 2015, kulikuwa na ongezeko la asilimia tisa ya mihadarati iliyokamatwa. Hadi sasa hakuna irada ya kutosha ya kimataifa ya kukabiliana na mihadarati. Hali kadhalika takwimu zinaonyesha kuwa tokea Marekani na waitifaki wake waivamie na kuikalia kwa mabavu Afghanistan, nchi hiyo imeshuhudia ongezeko la ugaidi, ukosefu wa amani na pia ongezeko kubwa la uzalishaji wa dawa za kulevya.

Nchini Afghanistan kuna mabara ya kisasa kabisa ya kutayarisha na kuzalisha dawa za kulevya na ni wazi kuwa nchi za Magharibi zina uwezo wa kusambaratisha maeneo hayo ya kuzalisha dawa za kulevya lakini kwa sababu kadhaa hazijachukua hatua yoyote  katika suala hilo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliandaa kongamano la kimataifa la kupambana na dawa za kulevya mjini Tehran mwezi Machi.

Wanajeshi wa Marekani wakiwa katika mashamba ya afiuni nchini Afghanistan

Akizungumza katika kikao hicho, Abdul Ridha, Rahmani Fazli, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Iran alisema: "Iran imeandaa mazingira mazuri ya ushirikiano wa kiintelijensia na kioperesheni katika kukabiliana na dawa za kuelevya kieneo na kimataifa, lakini mafanikio ya Iran yatategemea ushirikiano wa karibu wa nchi zingine."

Hivi sasa maspika wa mabunge kadhaa ya dunia wamejumuika Moscow na hiyo ni fursa nyingine ya kufanikisha vita dhidi ya mihadarati.

Kama alivyosema Spika wa Bunge la Iran, kupambana na mihadarati kunahitaji ushirikiano wa kimataifa hasa baina ya nchi ambazo zinaathiriwa vibaya na kwa njia ya moja kwa moja na mihadarati. Amesema kuna haja ya kudhibiti chanzo cha dawa za kulevya na kwamba hilo litafanikiwa kwa ushirikiano wa nchi za eneo. 

Tags