Mar 06, 2018 07:58 UTC
  • UN yasema mauaji dhidi ya Waislamu wa Rohingya yanaendelea Myanmar

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imetahadharisha kuhusiana na kuendelea mauaji ya kizazi yanayofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya magharibi mwa nchi hiyo.

Hayo yamesemwa leo Jumanne na Andrew Gilmour, Naibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia masuala ya haki za binadamu na kuongeza kuwa, "matokeo ya safari yangu ya hivi karibuni ya siku nne katika kambi za wakimbizi wa Kirohingya nchini Bangladesh yanaonyesha kuwa, Waislamu wa jamii hiyo ya walio wachache nchini Myanmar wangali wanakabiliwa na mauaji yaliyoratibiwa kwa ajili ya kuitokomeza jamii hiyo kikamilifu."

Amesema vyombo vya usalama vinatumia mbinu mpya kuwaangamiza Waislamu wa Rohingya, kama vile kuhakikisha kuwa hawapati chakula kwa kipindi kirefu, jambo ambalo linawalazimisha makumi ya maelfu miongoni mwao wakimbilie usalama wao nchini Bangladesh.

Waislamu wa Rohingya wakikimbilia Bangladesh

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka huu hadi sasa. 

Mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu nchini Myanmar yamepelekea zaidi ya Waislamu laki saba kukimbilia hifadhi katika nchi jirani ya Bangladesh.

Tags