Akthari ya Wamarekani: Mambo katika Ikulu ya White House yanaendeshwa shaghalabaghala
https://parstoday.ir/sw/news/world-i43992-akthari_ya_wamarekani_mambo_katika_ikulu_ya_white_house_yanaendeshwa_shaghalabaghala
Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni nchini Marekani yanaonyesha kuwa raia wengi wa nchi hiyo wanahisi hali katika Ikulu ya White House inakwenda shaghalabaghala.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 03, 2018 10:11 UTC
  • Akthari ya Wamarekani: Mambo katika Ikulu ya White House yanaendeshwa shaghalabaghala

Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni nchini Marekani yanaonyesha kuwa raia wengi wa nchi hiyo wanahisi hali katika Ikulu ya White House inakwenda shaghalabaghala.

Uchunguzi huo wa maoni uliofanywa na taasisi ya Politiko ikishirikiana na ile ya Morning Consult na matokeo yake kutangazwa hapo jana umeonyesha kuwa asilimia 62 ya Wamarekani waliotoa maoni yao wanaitakidi kwamba mambo katika Ikulu ya White House yanaendeshwa ndivyosivyo.

Hii ni katika hali ambayo katika uchunguzi kama huo wa maoni uliofanywa mwanzoni mwa mwezi Machi, asilimia 54 ya waliotoa maoni yao walikuwa na mtazamo huo.

Asilimia 49 ya watu waliotoa maoni yao aidha wanaitakidi kuwa rais wa nchi hiyo Donald Trump ameonyesha utendaji dhaifu katika kuteua wafanyakazi wapya na wenye sifa katika Ikulu ya White House.

Rais Donald Trump ambaye Wamarekani wengi wanaitakidi hayuko makini kiakili kuendesha nchi  

Uchunguzi huo wa maoni uliotangazwa na taasisi ya Politiko na Morning Consult ulifanywa baina ya tarehe 26 Aprili hadi Mei Mosi kwa kuwashirikisha watu 1,991 waliotimiza masharti ya kupiga kura.

Uchunguzi mwengine wa maoni uliofanywa karibuni na taasisi ya masuala ya umma ya Marekani NORC unaonyesha kuwa asilimia 60 ya vijana wa Marekani wanamwona Trump kuwa ni mtu mbaguzi na asiye makini kiakili kwa ajili ya kuendesha nchi..../