Sisitizo la Putin na Macron la kulindwa mapatano ya JCPOA
Akizungumza mara tu baada ya kuonana na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Rais Vladimir Putin wa Russia amesisitiza juu ya umuhimu wa kulindwa mapatano ya nyuklia kati ya Iran na nchi kubwa za dunia, mashuhuri kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kuusifu msimamo wa Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya kuhusiana na kudumishwa utekelezaji wa mapatano hayo.
Huku akisema kuwa hakuna sababu yoyote ya kufutiliwa mbali mapatano hayo, Rais Putin ametahadharisha kuwa matokeo ya kufutiliwa mbali mapatano hayo yatakuwa mabaya sana. Kwa uapande wake Rais Macron wa Ufaransa amesema kuwa licha ya uwezekano wa mashirika ya Ulaya kuwekewa vikwazo na Marekani, lakini yangali yana hamu ya kuendeleza mikataba yao ya kibiashara na Iran na kwamba mashirika hayo yanapasa kuipa Iran dhamana ya kudumisha mikataba hiyo nchini. Licha ya kuwa Macron amefanya safari nchini Russia kwa kisingizio cha kushiriki katika kongamano la kimataifa la masuala ya uchumi huko St. Petersburg, lakini ukweli wa mambo ni kuwa amefanya safari hiyo kwa ajili ya kubadilishana mawazo na Rais Putin kuhusiana na masuala muhimu ya kimataifa na hasa mapatano ya JCPOA, mzozo wa Ukraine na hali ya Syria. Bila shaka JCPOA ni suala muhimu zaidi kati ya masuala hayo matatu yaliyojadiliwa na viongozi hao wa Ufaransa na Russia.
Tangazo la Rais Ddonald Trump wa Marekani la kuiondoa nchi yake katika mapatano ya JCPOA hapo tarehe 8 mwezi Mei na sisitizo lake la kurejesha vikwazo dhidi ya Iran, halikuwarishidha wanachama wengine wa kundi la 5+1. Mara tu baada ya tangazo hilo Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya alipinga hatua hiyo ya Trump na kusisitiza kuwa Ulaya itaendelea kushirikiana na Iran katika utekelezaji wa mapatano hayo muhimu ya kimataifa. Nchi tatu muhimu za Ulaya yaani Ufaransa, Uingereza na Ujerumani pamoja na China na Russia zilitangaza wazi kuwa zitaendelea kubakia katika mapatano hayo. Inaonekana wazi kuwa kuongezeka pengo ka hitilafu kati ya nchi za pande mbili za Bahari ya Atlantic kuhusiana na masuala ya biashara, hali ya tabianchi (mazingira), nafasi ya nchi za Ulaya katika muungao wa kijeshi wa Nato na hivi sasa suala la JCPOA, limepelekea nchi za Ulaya kuhisi kuwa karibu zaidi na Russia kuliko wakati mwingine wowote. Umoja wa Ulaya na hasa nchi muhimu katika umoja huo kama Ujerumani na Ufaransa zimekasirishwa sana na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Russia, na kuendelea kutekelezwa vikwazo hivyo na hasa kuhatarishwa uhusiano wa nishati kati ya Ulaya na Russia kutokana na upinzani wa Marekani juu ya ujenzi wa bomba la gesi linalojulikana kama Nord Stream-2 ni jambo ambalo haliuridhishi kabisa umoja huo.
Ulaya ambayo sasa iko chini ya mashinikizo makubwa kutoka kwa Iran ambayo inaitaka itekeleze na kulinda kivitendo mapatano ya JCPOA na wakati huohuo kupunguza madhara ya utekelezwaji wa hatua ya kwanza na ya pili ya vikwazo vya Marekani dhidi ya serikali ya Tehran, inafanya kila linalowezekana kushirikiana na wanachama wengine wa kundi la 5+1 yaani Russia na China kwa lengo la kulemaza juhudi za Marekani za kutaka kudhoofisha na hatimaye kupelekea kufutiliwa mbali mapatano hayo ya kimataifa. Nchi za Ulaya huku zikisisitiza udharura wa kulindwa mapatano hayo ya nyuklia zimesema kuwa zitaendelea kubakia katika mapatano hayo. Nchi hizo zinaelewa vyema kuwa hazina kisingizio chcochote cha kujitoa katika mapatano hayo. Akizungumzia suala hilo Macron amesema: Maelezo ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) yanabainisha wazi kwamba Iran imetekeleza ahadi zake zote kuhusiana na mapatano ya JCPOA na kwa msingi huo nchi za Ulaya pia zinasisitiza kulindwa mapatano hayo. Mwisho wa kunukuu.
Katika upande wa pili, Putin naye ana sababu zake za kusisitiza kulinwa mapatano hayo. Kwa mtazamo wake, kuvunjwa mapatano hayo kutakuwa na matokeo mabaya sana, muhimu zaidi kukiwa ni kuenea ghasia na machafuko katika upeo wa kieneo na kimataifa. Kwa mtazamo wa Moscow hatua ya kujiondoa Marekani katika mapatano ya JCPOA kunatokana na siasa za upande mmoja za nchi hiyo. Rais Putin anasema: Russia kamwe haiungi mkono hatua za upande mmoja na kwa msingi huo haijawahi kuiwekea nchi yoyote ile vikwazo vya upande mmoja. Kila vikwazo vinapaswa kuwekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la sivyo hatua nyingine zozote zinatekelezwa kinyume cha sheria. Mwisho wa nukuu.
Nukta muhimu hapa ni kwamba, kinyume na alivyo Macron, Putin anapinga kuingizwa masuala ya pembeni kama vile makombora ya Iran na nafasi yake katika matukio ya Mashariki ya Kati, katika mazugumzo ya JCPOA. Kwa mtazamo wa Putin kushinikizwa Iran kuhusiana na masuala hayo kutapelekea kusambaratika kwa mapatano ya JCPOA.