Utafiti: US imeshadidisha matumizi ya drone katika utawala wa Trump
Utafiti mpya unaonesha kuwa, matumizi ya ndege zisizo na rubani (drone) za Marekani zenye silaha hatari yameongezeka katika utawala wa Donald Trump.
Utafiti huo uliofanywa na shirika la Stimson Centre umesema Marekani imeongeza kwa kiwango cha kutisha mashambulizi ya drone katika kufanya kufanya mauaji katika nchi mbalimbali.
Utafiti huo umebainisha kuwa, Trump ameagiza kwa akali hujuma 80 za drone katika mwaka wake wa kwanza ofisini, katika nchi za Waislamu za Pakistan, Yemen na Somalia.
Utafiti wa Stimson Centre umesema Trump ameagiza kufanyika mashambulizi hayo hatari ya ndege za US zisizo na rubani pasi na kuomba ushauri au ridhaa ya maafisa usalama wa nchi hiyo.
Ikulu ya Marekani ya White House enzi za Barack Obama ilikiri kuwa ndege zisizo na rubani za nchi hiyo zimeua idadi kubwa ya raia wasio na hatia katika nchi mbali mbali duniani na hususan za Kiislamu.
Shirika la Kijasusi la Marekani CIA limekuwa likitumia ndege hizo kutekeleza hujuma na ujasusi katika nchi za Afghanistan, Pakistan, Somalia, Yemen na Syria kwa kisingizio cha kukabiliana na makundi ya kigaidi.