Sep 11, 2018 13:54 UTC
  • Marekani yakosolewa kwa kuitolea vitisho mahakama ya ICC

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameikosoa vikali Marekani kwa kuishambulia na kutishia kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, baada ya korti hiyo yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi kusema kuwa itawafungulia mashitaka wanajeshi wa Marekani waliohusika katika jinai za kivita nchini Afghanistan.

Sima Samar, Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu nchini Afghanistan amesema ni jambo la kusikitisha kuona Marekani ikitoa vitisho dhidi ya majaji wa ICC ambao wanataka kuhakikisha kuwa wahanga wa jinai za wanajeshi wa US nchini Afghanistan wanapata haki, jambo ambalo litatoa mchango mkubwa kwenye mchakato wa amani nchini humo.

Naye Ehsan Qaane, afisa wa asasi ya kiraia ya Transitional Justice Coordination Group yenye makao yake mjini Kabul amesema suluhu ya kumaliza vita nchini humo ni kuwajibishwa watenda jinai wote, iwe ni wanajeshi wa Marekani au magaidi wa Afghanistan.

Jana Jumatatu, mshauri wa masuala ya usalama wa Ikulu ya Marekani White House, John Bolton alisema katu Washington haitashirikiana na ICC, huku akitishia kuwa Marekani itawawekea vikwazo majaji wa mahakama hiyo ya kimataifa, wanaotazamiwa kufuatilia mafaili ya jinai za wanajeshi wa US na maafisa wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA waliotenda jinai za kuogofya dhidi ya raia wa Afghanistan.

Mshauri wa masuala ya usalama wa Ikulu ya Marekani White House, John Bolton

Februari mwaka huu, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ilipokea mafaili milioni moja na laki saba ya jinai za kivita kutoka kwa wananchi wa Afghanistan, watuhumiwa wakuu wa jinai hizo wakiwa ni Marekani na kundi la kigaidi la Taliban.

Hadi sasa karibu askari elfu 14 wa kigeni wakiwemo elfu 11 kutoka Marekani wapo nchini Afghanistan. US iliivamia Afghanistan Oktoba mwaka 2001 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, wiki chache baada ya shambulizi la Septemba 11.

Tags