Trump kuwapa kibali wanajeshi kuwapiga risasi wahamiaji katika mpaka wa Mexico
Rais wa Marekani Donald Trump ameonya kuwa, maelfu ya wanajeshi wa nchi hiyo watakaotumwa katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico huenda wakalazimika kuwapiga risasi wahajiri wanaotoka katika nchi za Amerika ya Kati na wanaotaka kuingia Marekani kupitia mpaka huo.
Trump amesema amepokea habari kuwa msafara huo wa wahajiri umewarushia mawe askari polisi wa Mexico na kwamba jeshi la Marekani halitaruhusu jambo hilo kufanyika na ikibidi litawapiga risasi wahajiri wataowarushia mawe askari wa US.
Trump amesema serikali yake itatuma wanajeshi 15,000 kwenda kukabiliana na makumi ya maelfu ya wahajiri hao wanaotaka kuingia Marekani kupitia mpaka wa Mexico. Hii sio mara ya kwanza kwa Trump kuonesha chuki na muamala mbaya kwa wahajiri na wahamiaji haramu.
Hivi karibuni rais huyo wa Marekani alitoa matamshi mabaya yenye kuwavunjia heshima wahajiri au wahamiaji nchini humo kwa kuwataja kuwa ni wanyama, miezi michache baada ya serikali yake kuchukua hatua za kivitendo za kuwatenganisha watoto wahajiri na wazazi wao.
Wataalamu wa masuala ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamekosoa kitendo cha Marekani kuendelea kuwazuilia wahamiaji na raia wa kigeni wanaotafuta hifadhi nchini humo.
Novemba mwaka 2016 na hata kabla ya kuapishwa, Trump aliahidi kutekeleza ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi, likiwemo suala la kuwatimua wahamiaji milioni 3 nchini humo.