Nov 03, 2018 14:39 UTC
  • AI: Kadhia ya Khashoggi imedhihirisha unafiki wa Wamagharibi kuhusu Saudia

Msemaji wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International amesema kuwa mauaji ya kikatili ya mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi yamedhihirisha wazi unafiki wa Ulaya na Marekani kuhusiana na haki za binadamu nchini Saudi Arabia.

Ghias Aljundi ameviambia vyombo vya habari kwamba, watu wengi duniani wanajua vyema ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanyika nchini Saudi Arabia hususan baada ya Bin Salman kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo, lakini Ulaya na Marekani zinanyamazia kimya masuala hayo kutokana na mikataba ya silaha na uwekezaji wa serikali ya Riyadh. 

Ghias Aljundi ameongeza kuwa, mauaji ya kinyama ya Jamal Khashoggi yamedhihirisha unafiki huo mkubwa na sasa Marekani na nchi za Ulaya zinakabiliwa na mtihani mkubwa kwa sababu mauaji hayo ya kikatili si jambo linaloweza kunyamaziwa kimya.

Mwandishi na mkosoaji wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi aliuawala na maafisa wa utawala wa Riyadh tarehe Pili Oktoba baada tu ya kuingia katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul.

Saudi Arabia inaendelea kukaidi wito wa jamii ya kimataifa unaoitaka Riyadh ikabidhi maiti ya mwandishi huyo wa habari aliyeuawa na kukatwa vipande vipande na kisha maiti yake ikapelekwa kusikojulikana.

Tags