Russia: Marekani inawapa hifadhi magaidi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu Syria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50318-russia_marekani_inawapa_hifadhi_magaidi_katika_maeneo_yanayokaliwa_kwa_mabavu_syria
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema Marekani inakwamisha juhudi za kutatua mgogoro wa Syria kwa kuendelea kuyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na kwamba magaidi wanapewa hifadhi katika maeneo yanayodhibitiwa na Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 21, 2018 05:10 UTC
  • Russia: Marekani inawapa hifadhi magaidi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu Syria

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema Marekani inakwamisha juhudi za kutatua mgogoro wa Syria kwa kuendelea kuyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na kwamba magaidi wanapewa hifadhi katika maeneo yanayodhibitiwa na Marekani.

Maria Zakharova amesema kuwa, misaada na himaya ya jeshi la Marekani kwa magaidi wakiwemo wale wa Daesh huko kaskazini mwa Syria hususan karibu na kambi ya jeshi la Marekani ya Tanf ni jambo linalojulikana wazi na kwamba askari wa Marekani hawaruhusu mtu yeyote kuingia katika eneo hilo. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameongeza kuwa, njia pekee ya kukomesha mgogoro wa Syria ni kuunga mkono mazungumzo kati ya Wasyria wenyewe na kujiepusha na machafuko na utumiaji mabavu.

Maria Zakharova

Vilevile ameashiria jitihada zinazofanywa na Tehran, Moscow na Ankara kwa pamoja kwa ajili ya kutafuta suluhisho la mgogoro wa Syria kupitia vikao vya mazungumzo ya Astana na kusema kuwa: Hatua muhimu zaidi ilikuwa kushauriana kuhusu muundo wa tume ya kubuni katiba mpya ya Syria, suala ambalo limekamilika kupitia mazungumzo ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran, Russia na Uturuki na vilevile mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Syria, Staffan de Mistura. 

Zakharova amesema tume hiyo itaanza kazi zake mwanzoni mwa mwaka ujao na kubuni katiba mpya ya Syria kwa mujibu wa azimio nambari 2254 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.