Jan 17, 2019 07:48 UTC
  • Ripoti: Uchumi wa China kuupiku wa Marekani mwaka ujao

Ripoti ya Benki ya Standard Chartered imedokeza kuwa, kuna uwezekano mkubwa China kuipiku Marekani na kuwa nchi yenye uchumi mkubwa zaidi duniani mwaka ujao wa 2020.

Ripoti hiyo imesema kuwa, uchumi wa China unakuwa kwa kasi kubwa na miongoni mwa vigezo vitakavyoifanya iipiku Marekani na kuwa dola lenye uchumi mkubwa zaidi duniani kufikia mwaka ujao ni kuimarika kwa mapato yake ya taifa (GDP) na kutoyumba kwa sarafu ya nchi hiyo ya Asia ikilinganishwa na Marekani.

Ripoti hiyo ya Benki ya Standard Chartered imeongeza kuwa, Russia pia itazipiku Ujerumani na Uingereza na kuwa miongoni mwa nchi tano zenye uchumi mkubwa duniani, pamoja na India na Japan.

Mwaka uliomalizika wa 2018 China na Marekani ziliingia katika vita ya kibiashara ambapo wataalamu wa uchumi walionya kuwa, vinaweza kusababisha hasara kubwa kwa uchumi wa dunia

Mtafiti wa benki hiyo, Madhur Jha amesema kuwa, "Kufikia mwaka 2020, aghalabu ya nchi duniani zitakuwa katika orodha ya nchi zenye kipato cha wastani, hususan nchi za bara Asia. Nchi saba za Asia zitakuwa katika orodha ya nchi 10 zenye chumi kubwa zaidi duniani, na kuzipiku nchi za Magharibi kufikia mwaka 2030." 

Hivi karibuni Rais Vladmir Putin wa Russia alisema kuwa, Moscow na Beijing zimekusudia kutumia sarafu zao za kitaifa katika miamala ya kibiashara, badala ya kutumia sarafu ya Dola ya Marekani, kwa kuzingatia mizozo iliyopo kati ya Russia na nchi za Magharibi.

Tags