Apr 23, 2019 14:23 UTC
  • Kundi la Daesh (ISIS) latangaza kuhusika na mashambulizi ya Sri Lanka

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) limetangaza kuwa ndilo lililohusika na miripuko ya mabomu ya hivi karibuni nchini Sri Lanka, iliyoua mamia ya watu.

ISIS imeyasema hayo leo Jumanne kupitia shirika lake la habari za kipropaganda la Amaq.

Hata hivyo genge hilo la kitakfiri halijatoa maelezo ya kina wala ushahidi wowote wa kuonesha kuwa ndilo lililohusika na hujuma hizo.

Hii ni katika hali ambayo, vyombo vya usalama nchini humo vimeripoti kuwa, mashambulio hayo ya Jumapili iliyopita yalifanywa na magenge ya kigaidi ya nchi hiyo. 

Kadhalika wapelelezi wanasema wanachunguza iwapo waliotekeleza hujuma hizo za kigaidi wana uhusiano wowote na mitandao ya kimataifa. 

Athari za hujuma za Daesh kanisani nchini Sri Lanka

Huku hayo yakiarifiwa, idadi ya watu waliopoteza maisha katika hujuma hizo za kigaidi nchini Sri Lanka imeongezeka na kufikia watu 321. 

Msemaji wa polisi nchini Sri Lanka amesema hadi sasa watu 500 wamethibitishwa kujeruhiwa katika hujuma hizo za kigaidi ambazo zililenga makanisa matatu, hoteli nne za kifahari na nyumba.

Tags