Jitihada za Marekani za kuzidisha mivutano katika eneo la Asia magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i53715-jitihada_za_marekani_za_kuzidisha_mivutano_katika_eneo_la_asia_magharibi
Rais Donald Trump wa Marekani tangu aingie madarakani amekuwa akitoa zingatio makhusi kwa eneo la Asia Magharibi na khususan eneo la Ghuba ya Uajemi; na hata safari yake ya kwanza nje ya nchi ilikuwa nchini Saudi Arabia, ili kuonyesha umuhimu wa eneo hili katika siasa za nje za Marekani na nafasi ya washirika wa Washington katika eneo. Bila shaka Trump mara kadhaa amekuwa akiutaja utawala wa Saudia kuwa ni ng'ombe wa kukamwa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 26, 2019 02:25 UTC
  • Jitihada za Marekani za kuzidisha mivutano katika eneo la Asia  magharibi

Rais Donald Trump wa Marekani tangu aingie madarakani amekuwa akitoa zingatio makhusi kwa eneo la Asia Magharibi na khususan eneo la Ghuba ya Uajemi; na hata safari yake ya kwanza nje ya nchi ilikuwa nchini Saudi Arabia, ili kuonyesha umuhimu wa eneo hili katika siasa za nje za Marekani na nafasi ya washirika wa Washington katika eneo. Bila shaka Trump mara kadhaa amekuwa akiutaja utawala wa Saudia kuwa ni ng'ombe wa kukamwa.

Serikali ya Trump katika siku za karibuni imeshadidisha hali ya mivutano katika eneo la Asia Magharibi. Katika uwanja huo, baada ya Pentagon kutuma katika eneo la Ghuba ya Uajemi manowari ya Abraham Lincoln, ndege za kivita za kistratejia aina ya B-52 na ngao za makombora za Patriot; hivi sasa Trump ametangaza habari ya kutumwa katika eneo  wanajeshi wapya wa Marekani. Trump juzi Ijumaa alitangaza kuwa Marekani imetuma wanajeshi wake wapya 1500 katika eneo la Asia Magharibi na kusitiza kuwa wanajeshi hao wametumwa katika eneo eti ili kujilinda.

Serikali ya Trump imetuma wanajeshi hao wapya katika hali ambayo akiwa katika kampeni zake za uchaguzi; Trump alimkosoa rais aliyemtangulia kwa kutuma wanajeshi katika eneo na kuahidi kwamba angewarejesha nyumbani iwapo angeshinda uchaguzi. Huku ikiwa na lengo la kudhihirisha kuwa hatua hiyo ni yenye umuhimu mdogo; Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imetangaza kuwa mafundi na wahandishi ni miongoni mwa wanajeshi wa ziada wa nchi hiyo ambao wanatumwa katika eneo la Asia Magharibi. Kama ilivyokiri Wizara hiyo ya Ulinzi ya Marekani; kati ya wanajeshi 1500 ambao wametumwa Asia Magharibi,  wanajeshi 900 ni wapya na 600 wengine tayari wapo katika eneo; ambapo muda wao wa kuhudumu utaongezwa. Hatua hiyo ya Trump imepingwa vikali ndani na nje ya nchi. Adam Smith Mwenyekiti wa Kamati ya Vikosi ya Ulinzi katika Bunge la Wawakilishi la Marekani juzi Ijumaa alilalamikia uamuzi huo wa Trump wa kutuma wanajeshi zaidi katika eneo eti kwa lengo la kusambaratisha vitisho vya Iran. Smith ameutaja uamuzi wa Pentagon wa kuongeza idadi ya wanajeshi katika eneo la Asia Magharibi kuwa wenye kutia "wasiwasi" na kueleza kuwa: Kuzidisha idadi ya wanajeshi bila ya kuwa na stratejia ya wazi ni hatua isiyo ya kimantiki; na hiyo ni hatua ya wazi na ya mabavu yenye lengo la kushadidisha hali ya mivutano na Iran. 

Adam Smith, Mwenyekiti wa Kamati ya Vikosi vya Ulinzi katika Bunge la Wawakilishi Marekani 
 

Hatua hii ya karibuni ya Washington ya kuongezea idadi ya wanajeshi wake Asia Magharibi imechukuliwa kwa kisingizio cha kuwepo vitisho kutoka kwa Iran dhidi ya wanajeshi wa Marekani na vile vile eti kutokana na kuwepo hatarini maslahi ya washirika wa Marekani katika eneo. Pamoja na hayo, inaonekana kuwa Washington inafanya kila linalowezekana ili kufanikisha kivitendo malengo yake iliyoyakusudia kwa kuidhihirisha Iran kuwa ni tishio sambamba na kuzidisha uuzaji wa silaha zake kwa waitifake wake kwa kuzidisha hali ya mivutano katika eneo. 

Mfano wa wazi wa jitihada hizo ni pale Ijumaa ikulu ya Marekani (White House) ilipotangaza kuwa ina mpango wa kuziuzia silaha Saudia na Imarati  bila ya kibali cha kongresi ya nchi hiyo. Kwa utaratibu huo, serikali ya Trump imepuuza sheria ya kongresi huku ikiharakisha mchakato wa kuziuzia Saudia na nchi nyingine silaha za mabilioni ya dola. Maseneta kadhaa wa Marekani akiwemo Bob Menendez wa chama cha Democrat katika seneti ya nchi hiyo wamesema kuwa: Serikali ya Trump  imezijulisha rasmi kamati za kongresi kuhusu utekelezaji wa makubaliano 22 ya mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia na Imarati yenye thamani ya dola bilioni nane.  Pamoja na hayo, hatua hizi za Washington hazijabaki hivi hivi bila jibu bali zimekabiliwa na radiamali ya Russia ikiwa nchi mshindani wa Marekani kimataifa. Maria Zakharova Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema: Hatua za chokochoko za Washington dhidi ya Tehran zinaweza kuibua makabiliano yasiyo na mwisho ambayo huenda yakawa na taathira mbaya. Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetangaza kuwa kuna uwezekano hatua hizo za Marekani zikajadiliwa katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia