Jul 05, 2019 06:45 UTC
  • Kufichuliwa nafasi ya Marekani katika kusimamishwa meli ya mafuta ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Hispania amefafanua habari mpya inayohusiana na hatua ya kusimamishwa meli iliyokuwa imebeba mafuta ya Iran katika eneo la Jabal at-Twariq (Gibraltar).

Joseph Borrell, Waziri wa Mambo ya Nje wa Hispania, amesema kuwa wanamaji wa Uingereza walichukua hatua ya kuisimamisha meli hiyo katika maji ya Jabal at-Twariq baada ya kupata ombi kutoka kwa serikali ya Marekani. Waziri huyo wa mambo ya nje wa Hispania amesema kuwa kutokana na kuwa kidhahiri meli hiyo iliyokuwa imebeba mafuta ya Iran ilisimamishwa ikiwa katika maji ya nchi hiyo katika eneo la Jabal at-Twariq, serikali ya Madrid inachunguza suala hilo kwa shabaha ya kuwasilisha rasmi malalamiko yake kwa vyombo husika. Meli hiyo ilisimamishwa katika maji ya eneo lililotajwa ambalo Uhispania haitambui rasmi mamlaka ya Uingereza juu yake.

Viongozi wa Jabal at-Twariq walitoa taarifa wakitangaza kuwa walikuwa wameisimamisha meli hiyo kwa jina la Grace 1 Alhamisi asubuhi na kudai kuwa ilikuwa ikisafirisha mafuta kuelekea kiwanda kimoja cha kusafisha mafuta nchini Syria.

Joseph Borrell, Waziri wa Mambo ya Nje wa Hipania

Kufuatia hatua hiyo isiyo ya kisheria ya kikosi cha wanamaji wa Uingereza, balozi wa nchi hiyo mjini Tehran aliitwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku hiyo hiyo ya Alhamisi ili kukabidhiwa malalamiko rasmi ya Iran kuhusiana na suala hilo.

Balozi huyo amekabidhiwa nyaraka zote zinazohusiana na meli hiyo na mafuta iliyosheheni zinazothibitisha kwamba haikuwa imevunja sheria yoyote ya kimataifa wala ya sehemu iliyokuwa ikipita.

Tags